Watu 12 wamejeruhiwa wakati wa mashambulizi ya kurushiana risasi
baina ya askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) Kikosi 128 KJ cha Nyandoto
na Polisi wa Kituo cha Stendi wilayani Tarime mkoani Mara.
Hatua hiyo imekuja wakati wanajeshi hao walipokuwa
wakijaribu kumchukua askari mwenzao aliyekamatwa na Polisi wa Kikosi
cha Usalama Barabarani kwa kuendesha pikipiki bila kuwa na kofia ngumu.
Mashambulizi hayo ya kurushiana risasi na kutwangana ngumi na mateke yalitokea juzi saa 12 jioni katika Kituo cha Polisi Stendi.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji
wa Tarime, Bernard Makonyo alisema amepokea majeruhi 10, kati ya hao
wawili ni askari wa JWTZ, polisi saba na raia mmoja. Alisema majeruhi
tisa wameruhusiwa na mwingine kupelekwa Hospitali ya Shirati kwa
matibabu zaidi.
Dk Makonyo aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Aloyce
Filbert (24) aliyepigwa risasi mguu wa kulia, Deodatus Dominic (26)
aliyejeruhiwa puani na wote ni askari wa JWTZ.
Wengine ni askari polisi saba ambao ni Makoye
Katula (26), Sylvester Michael (31), Salum Omary (44), Abdallah Halifa
(24), Joel Msabila (25), Ally Juma (27) na Deogratius Tryphon (32) na
raia Hamza Jumanne (33) aliyepigwa risasi mguu wa kushoto ambaye
alipelekwa Hospitali ya Shitari, Rorya kwa matibabu.
Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi
Tarime/Rorya, Ndalama Salumu anadaiwa kujeruhiwa kwa kupigwa katika
vurumai hizo huku mwananchi mwingine, David Kisaro (20) akijeruhiwa kwa
bomu jichoni. Alitibiwa katika Zahanati ya Tarime.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya,
Benedict Mambosasa alisema mwanajeshi aliyekamatwa alifanya makosa kwani
baada ya kukamatwa na kuombwa kwenda kituo cha polisi, alikaidi.
Mambosasa alisema mwanajeshi huyo licha ya kukiuka
taratibu, aliwatolea lugha za matusi polisi jambo lililowalazimu
kumkamata kwa nguvu, ndipo wanajeshi wenzake walipoingilia kati na
kusababisha kutokea kwa majibishano ya risasi za moto. Hata hivyo,
alisema hakuna aliyejeruhiwa.
Alisema wanajeshi watatu ambao hawakutajwa majina, wamekamatwa na polisi kwa kuvunja utaratibu wa usalama.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, amelaani
kitendo hicho cha kurushiana risasi za moto hewani akisema ni cha utovu
wa nidhamu na maadili ya kazi ya jeshi na kwamba hatua kali
zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema wananchi Tarime wameshangazwa kwa kitendo
kilichofanywa na walinda usalama hao, wakisema si cha kinidhamu huku
wakisema kilikwamisha shughuli zao kwa muda kwa kuhofia usalama wa
maisha yao.
Mkazi wa Tarime, Joseph Samson amesema kitendo hicho kimewashangaza sana wananchi
Mkazi wa Tarime, Joseph Samson amesema kitendo hicho kimewashangaza sana wananchi