KAMPUNI ya
ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ikiwa chini ya
uongozi wa kampuni ya Pan African Power Solutions (T) Limited (PAP) imetangaza
kufikia kwa punguzo la bei ya umeme la asilimia 20 baada ya kufanya marekebisho
makubwa ya injini za mtambo huo ya masaa 36,000 ikifanya kazi, zoezi
iliyokamilika ndani ya mwanka 2014. IPTL pia
imetangaza kuwa bei yao ya umeme ikitarajiwa kushuka zaidi kulingana na kushuka
kwa bei ya mafuta mazito.
Marekebisho
hayo yaliyotumia zaidi ya Dola za kimarekani milioni 25 yameiwezesha mitambo ya
IPTL kuwa katika nafasi nzuri ya kuzalisha umeme wa uhakika kwa kufikia megawati
100 na kuingiza katika gridi ya Taifa mara to baada ya kukamilika kwa zoezi
hilo mnamo Desemba mwaka 2014.
Kwa mujibu
wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni hiyo, Bw. Harbinder
Singh Sethi, IPTL sasa imepunguza bei ya umeme wake inaoutoza kwa Shirika la
ugavi wa umeme Tanzania (Tanesco) ambao sasa utakuwa chini ya bei ya awali
iliyokokotolewa ya senti 23 dola za kimarekani kwa Kilowati; huku ikihakikisha
kupatikana kwa umeme wa uhakika.
"Tukiwa
tunaukaribisha mwaka 2015, IPTL inajivunia kutangaza kuwa imefanikiwa kufanya marekebisho
makubwa ya mashine zake ya masaa 36,000 ya kufanya kazi, zoezi iliyokamilika
ndani ya mwaka wa 2014. Nimeiomba timu ya IPTL kupanga mapema jinsi gani
wanaweza kuongeza juhudi zaidi kufikia marekebisho ya masaa 48,000, katika
awamu inayofuata katika mwaka 2015. Tunatarajia uwepo wa IPTL kuwa bora zaidi
kwa kuwa sasa tunajipanga kuongeza rasilimali zaidi.
"Hii
ni sehemu ya ahadi ya PAP kuhakikisha kuwa IPTL inaendeshwa vizuri na kwa
ufanisi. Wakati sasa umefika kwa TANESCO kuwa na uhakika wa kupata umeme wa
uhakika wa megawati 100 katika gridi ya taifa wakati wowote utakapohitajika.
"IPTL
chini ya PAP haiangalii tu uzalishaji wa umeme wa kutosha, lakini pia ipo
makini kuhakikisha kuwa umeme huo wa kutosha unakuwa nafuu. Kwa maana hiyo,
tumeamua kushusha bei zetu za umeme kufikia chini ya bei iliyokokotolewa ya
hapo awali ya senti 23 dola za kimarekani kwa uniti, ambayo sasa inaleta jumla
ya punguzo la bei la asilimia 20 kwa ile iliyokuwa ikitozwa na IPTL kabla
ya PAP kuchukua uongozi," alisema.
Bw. Sethi
aliongeza kuwa TANESCO itarajie punguzo zaidi la bei ya umeme kufikia kiwango
cha chini ya Senti 8 Dola za kimarekani kwa kila uniti ya umeme mara baada ya
mitambo ya IPTL kupanuliwa na kufikia uzalishaji wa megawati 500 mitambo yake
ikitumia gesi asilia.
Alisema
kuwa mpango wa upanuzi wa mitambo hiyo unaendelea vizuri, akiongeza kuwa iko
katika hatua za awali za uchanganuzi na upimaji wa udongo.
"Tunatarajia
hatua za upanuzi kwenda haraka ili kuhakikisha kuwa IPTL inatoa huduma bora, ya
uhakika na nafuu katika taifa hili. Ningependa kutoka shukrani zangu kwa
uongozi wa TANESCO na Gridi ya Taifa kwa kukubali umeme unaozalishwa na
IPTL,"alisema.
Kwa mujibu
wa vyanzo mbali mbali kutoka TANESCO, bei za umeme zinazotozwa na IPTL kwa sasa
zimeshuka na kufikia chini ya Senti 19 Dola za kimarekani kwa uniti za umeme
kutokana na kushuka kwa bei ya Mafuta mazito wakati wa kipindi cha ukokotoaji
wa bei hizo.
Upatikanaji
wa umeme wa uhakika kutoka IPTL tayari umeshathibitika wakati wa kipindi cha
sikukuu kilichopita ambapo nchi haikukumbana na mgawo wowote ikilinganishwa na
miaka iliyopita ambapo ilikuwa ni kawaida kwa umeme kukatika katika wakati wa msimu
wa sikukuu ambapo kunakuwa na mahitaji makubwa.