Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.
Na Mwandishi Wetu
HAPATOSHI! Siku moja baada ya
mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anayewakilisha Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo
kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) sasa imebainika kuwepo kwa
shughuli pevu kati yake na Dk. John Pombe Magufuli, anayesimama kwenye
‘vita’ hiyo kuwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli.
Dk. Magufuli alichukua fomu hizo Jumanne
iliyopita katika hafla iliyokusanya maelfu ya wakazi wa Jiji la Dar es
Salaam na vitongoji vyake, hivyo kutokana na umati ambao pia Lowassa
aliupata jana, upinzani mkali unatarajiwa katika majukwaa ya makada hao
wawili ambao walikuwa pamoja CCM wakati wa kampeni zitakazohitimishwa
kwa uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
Barabara zote alizopita Lowassa zilijaa
mashabiki wa Ukawa huku baadhi ya watu wakisema kwamba umati huo ni
kama jino kwa jino na ule wa Dk. Magufuli siku aliyokwenda kuchukua
fomu.
“Kwa kweli uchaguzi wa mwaka huu utakuwa
ni shughuli pevu kweli kweli kati ya wagombea hawa wawili, maana
ukitazama siku ya uchukuaji fomu, unagundua kuwa wote wana nguvu
zinazokaribiana, kuna hatari ya mtu kupata matokeo yasiyotarajiwa kama
atadharau upande mwingine,” alisema mfuasi mmoja wa CCM, aliyehudhuria
hafla za wagombea wote wawili walipochukua fomu Nec.
Hata hivyo, mgombea wa CCM, Dk. Magufuli
anapewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda uchaguzi huo kutokana na
historia yake ya utendaji katika nafasi mbalimbali alizopewa tangu
serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin William Mkapa, kwani
amejipambanua kuwa ni mchapakazi anayeweza kuvunja makundi ndani ya
chama hicho tawala.
Lowassa, Mbunge wa Monduli atapeperusha
bendera ya Ukawa unaoundwa na vyama vinne vya Chadema, Cuf, NCCR-Mageuzi
na NLD, ambao hata hivyo umegubikwa na sintofahamu baada ya Mwenyekiti
Mwenza, Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu uongozi wa chama chake huku
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa akijiweka kando tangu ujio wa
waziri huyo mkuu wa zamani.
credit: GPL