Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
NASHANGAA, kwa
nini msomi kama Prof. Ibrahim Haruna Lipumba anatafuta uongo kuuficha
utashi wake ambao kimsingi ndiyo uliomfanya awe mwanamageuzi na kukubali
kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (Cuf)?
Usomi siyo kuwa na vyeti ni uwezo au
maarifa ya kukabiliana na changamoto za maisha. Nilitaraji kumuona Prof.
Lipumba akifikia tafsiri hii baada ya kubaini kuwa Umoja wa Katiba ya
Mwananchi (Ukawa) alimokitumbukiza chama chake lilikuwa ni kosa
lililohitaji maarifa kulitatua.
“Nimeamua kujiondoa kwenye nafasi ya
uenyekiti kwa sababu wenzangu wameniona kuwa ni kikwazo…Watu walioipinga
katiba tuliyoipendekeza ndiyo tunaowapa nafasi ya kuongoza umoja wetu.”
Haya ni maneno ya Prof. Lipumba
aliyoyatoa wakati akijiuzulu wadhifa wake wa uenyekiti wa Cuf, maneno
ambayo sikuyapangilia ipasavyo kwa sababu nilichotaka kukiweka ni sura
tu ya namna alivyoachia ngazi.
Wakati akitangaza uamuzi huo sikuwepo
kwenye mkutano wake, nadhani hakuniita makusudi kwa sababu ananifahamu
kuwa mimi ni mbishi, sipendi kudanganywa, pengine ningemuuliza maswali
magumu ya kumchefua:
“Unajiondoa Ukawa au Cuf? Wewe siyo
mwenyekiti wa Ukawa ni wa Cuf! Kwa nini usikitoe chama chako kwenye
umoja huo haramu badala yake umejitoa wewe kana kwamba waliokupa kura ya
uwenyekiti ni hao Ukawa unaowakimbia?
“Huoni Prof. Lipumba kufanya hivi
kunakuondolea heshima mbele ya watu waliokuamini na kukupenda kwa miaka
zaidi ya 20 katika harakati zako? Unawezaje kuhama nyumba kwa kufukuzwa
na mpangaji mwenzako huku ukiwaacha wanao kwenye huzuni kubwa?”
Haya ndiyo maswali ambayo ningemuuliza
mfululizo Prof. Lipumba kwa sababu katika akili yangu sijaona mantiki ya
yeye kuachia cheo cha uenyekiti wa Cuf kwa sababu eti ameonekana
kikwazo cha Ukawa; kwani Ukawa ni Cuf na Cuf ni Ukawa?
Akili ya kawaida lazima ilete majibu ya
mshangao vinginevyo mwenyekiti huyo afanye masahihisho ya kauli yake kwa
kusema kuwa waliomuona kikwazo siyo Ukawa bali ni viongozi wenzake
ndani ya chama chake, hapo atakuwa na sababu ya kuachia ngazi ya
uenyekiti wa Cuf.
Ikiwa hivi ninavyosahihisha kauli ndivyo
ilivyo kwamba, Prof hakukubaliana na utaratibu wa chama chake kujiunga
Ukawa na viongozi wenzake wa chama wakaona ‘anawazingua’ kwa nini
asiseme wazi kuwa ameamua kuachia ngazi baada ya kupingana na viongozi
wenzake?
Kulikuwa na ubaya gani kuwaita waandishi
wa habari na kutamka hadharani kwamba, katibu mkuu wake, Maalim Seif
Sharrif Hamad, amempuuza na kwamba yeye hakuwa tayari kufanyiwa hivyo
kwa masilahi ya chama chake? Hapo angeieleza jamii jinsi alivyojitahidi
kutatua tatizo hilo, alivyowashirikisha wananchama waliomchagua na
namna ilivyoshindikana kiasi cha kufikia kuachia ngazi, hapo angeeleweka
na kila mtu!
Lakini kutoa hoja dhaifu kwamba hicho
ndicho kikwazo cha nafasi yake nyeti ndani ya chama, hawezi kukwepa
tuhuma kwamba amenunuliwa na chama tawala kwa lengo la kuhujumu Ukawa.
Hawezi kukwepa kejeli kwamba maisha ya
upinzani kayazoea na kwamba amekuwa hapendi kukiona chama chake kikiwa
na nguvu ya kushika dola.
Prof. Lipumba hatakaa ajisafishe na
mtazamo kuwa siasa za kashkashi ndani ya upinzani zilikuwa zimemlevya na
kwamba alikuwa anasubiri kusukumwa kidogo aanguke, puuu!
Nasikitika Prof. Lipumba amehama nyumba
kwa kufukuzwa na mpangaji mwenzake, ameamua kuwaacha wanachama
waliopigana kwa kumwaga damu katika changuzi mbalimbali na wengine ni
vilema mpaka sasa kwa sababu yake!
Ikiwa ni hivi, siasa na wanasiasa siyo watu wa kuwaamini hata kidogo. Nachochea tuna GPL