Wiki
iliyopita nilianza simulizi hii ya viumbe wa ajabu waitwao Aliens
waishio angani. Niliishia pale nilipoanza kueleza ni viumbe gani hawa
ambao wamekuwa wakihusishwa na upotevu wa watu na ndege duniani? SASA
ENDELEA…
Juu ya viumbe hawa wa ajabu waishio angani waitwao Aliens, mifano
mingi inayotolewa inalenga kuthibitisha kuwa kweli kuna viumbe wa ajabu
ambao wamekuwa wakishindana na binadamu bila wenyewe kujua hivyo kuwapa
kazi kubwa wanasayansi wa anga kufanya utafiti wa ziada.
Katika simulizi hii inaweza kuniwia vigumu kuthibitisha au kukiri
kuwa naamini uwepo wa viumbe hawa ila ninachojaribu kukifanya ni
kukutengenezea mazingira kuwa mbali na majini na mashetani, angani kuna
viumbe, bakteria, vitu na hata virusi ambavyo bado wanasayansi duniani
hawajavigundua.
Kumbuka; si kila kilichopo mtandaoni ni cha kweli. Hata wewe unaweza
kubuni simulizi za aina fulani na ukapata wafuasi wa kutosha. Kidogo tu
nithibitishe hilo kisha tuendelee na simulizi yetu. Kuhusu familia za
kitajiri au kifalme kumekuwa na stori kuwa hubadilika na kuwa reptilia.
Hizo ni stori tu na zipo nyingi ambapo hakuna uthibitisho kwa kuonekana
ni uchawi au mambo ya kishetani.
Kuna baadhi ya binadamu wanaoamini uwepo wa Aliens hasa baada ya
kutazama filamu nyingi za Kimarekani zilizobeba simulizi za viumbe hawa.
Kama ulifanikiwa kufuatilia Runinga ya ITV ya Tanzania, miaka kadhaa
iliyopita, kuna ‘series’ ya tamthiliya ilikuwa ikirushwa ya Babylon 5
iliyokuwa ikionesha maisha yanavyoendelea huko angani kuhusu hawa
Aliens.
Pia ipo sinema nyingine ya Kihindi ambayo inawahusu Aliens inayoitwa
Koi Milgaya au I Found Someone, nayo inathibitisha uwepo wa hawa viumbe
duniani japokuwa wapo wanaomini ni mambo ya kusadikika tu.
Kuna uthibitisho kwamba series za hawa Aliens, Vampires, Super
Heroes, Golins, Ware Wolves na zingine nyingi, ni kati ya vitu
vinavyopendwa kufuatiliwa na binadamu hasa kabla ya kulala kwa kuwa
zinaonesha maisha nje ya ulimwengu wa kawaida.
Mapitio ya baadhi ya wanasayansi yanaonesha kuwa mbali na Aliens
hakuna kiumbe kingine kilichogundulika nje ya sayari ya dunia.
Kilichobaki ni makisio kuwa huenda sayari zingine kuna uwezekano wa
kuwepo na uhai kulingana na hali ya hewa na dalili ya uwepo wa maji
ingawa bado haijathibitishwa 100%, mfano Mars.
Kama nilivyoeleza awali kuwa kuna sinema nyingi tunazoziona kuhusu
hawa Aliens ni maendeleo tu ya kisayansi ndiyo maana Hollywood, Marekani
wamepiga fedha na utajiri mkubwa huku mambo mengi yakiwa ni simulizi za
kufikirika.
Kuna watu wanaamini kuwa kila wanachosema Wamarekani katika sayansi
ni kweli. Si kweli. Ikumbukwe kuwa vitu visivyojulikana angani (UFO)
siyo viumbe na si kweli kwamba Wamarekani hawajui vile ni vitu gani.
Inaaminika kuwa UFO (Unidentified Flying Object) ni matokeo ya
maendeleo ya sayansi ya anga kati ya wanasayansi wa Kimarekani na hawa
Aliens na Wamarekani wanaujua ukweli juu ya jambo hilo.
Habari nyuma ya pazia ni kwamba wanasayansi wa Kimarekani hawataki
kabisa wanadamu wa kawaida wajue uhusiano wao na hawa Aliens kwa sababu
inaaminika ni mambo ya kishetani! Katika moja ya ripoti zao kupitia
Shirika la Utafiti wa Anga ya Juu la Marekani (NASA), wanasayansi hao
waliwahi kuripoti kwamba kwenye moja ya safari zao angani walipokuwa
wanakwenda kutua mwezini, njiani waliona chombo chenye viumbe hao wa
ajabu wa Aliens.
Itaendelea wiki ijayo, usikose