Haina Shida kuwa nazo hizo nyingi lakini mbona kuna ufanano fulani wa story? Inawezaka nimeangalia vibaya au kuna mapungufu sehemu fulani na/au watu wale wale wamekuwa wakicheza sehemu zile zile hivyo nashindwa kutofautisha story.
Ni juzi tu hapa kwenye vyombo vya habari nilibahatika kuona waigizaji wa hapa Bongo wakihojiwa. Kwanza aliwalalamika watunzi wa story hizo na pili kila mara kuchezeshwa sehemu zile zile mfano kama mtu amekuwa yuko vizuri kuwa baba wa familia utakuta kila mara ni hivyo huwezi kumkuta kwenye sehemu nyingine na kuwafanya washindwe kujua huyu mtu anawezaje kubadilisha story akifanya sehemu nyingine tofauti.
Nikirudi kwenye swali langu la msingi, je hakuna story nyingine zaidi ya mapenzi na uchawi? Mapenzi yametawala filamu zetu ingawa si kwamba hapa Bongo mapenzi yako hivyo kama yanavyoonyeshwa kwenye filamu zetu. Hiyo si ishu sana bali wasi wasi wangu ni kwamba waandishi wetu ni kama wamekosa ubunifu katika uandishi wao wa filamu au wanaona wakija na kitu kipya wanaweza wasiuze au hakiuziki sokoni.
Katika taaluma yoyote ubunifu ni jambo la msingi na huo ubunifu ukikosekana unakuwa unafanya kitu kile kile kila wakati, mwisho wa siku watu wanachoka. Inawezekana watazamaji hawajachoka au wamechoka ila hawana mbadala hivyo wanalazimika kuendelea kuwa wateja waaminifu kwasababu hakuna njia nyingine.
Kama watanzania wangekuwa na mbadala wa filamu za Bongo ambazo wakati mwingine ni zile za kinaijeria basi filamu zetu zinaweza kupotezwa mapema sana. Wale ambao wangeweza kuwa wabunifu na kuboresha uandishi wao ndio wanageuza lakini wengine soko lingewakataa kabisa. Swali langu la msingi ni kuwa hakuna story nyingine? Na kama zipo mbona ni chache tatizo ni nini?
Hivi ulishawahi kuwaza kama watanzania wengi wangekuwa wanajua Kiingereza kama Kiswahili kilivyo sasa unafikiri wangeangalia filamu gani zaidi?
Je! kizazi cha watoto hawa wa English medium unafikiri wakiona huna jipya wataifanyaje filamu yako? Tunahitaji mageuzi makubwa kwenye filamu zetu ili kwenda na wakati huku mkiongeza ubunifu wa hali ya juu ikiwezekana wapelekeni wandishi shule ili waongezee pale ambao elimu yao imeishia.
Ni mtazamo tu, tafakari na wahusika wachukue hatua za kimakusudi kabisa kututoa hapa tulipo.