Wabunge wa Ukawa wakitoka bungeni hapo jana.
WABUNGE wa vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) wameelezea sababu zilizowafanya wao
kuuchukua uamuzi wa kupiga kelele ndani ya bunge kuwa ni baada ya Rais
wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kuingia Bungeni hali iliyopelekea
kutolewa nje ya Bunge hilo.
Mbunge wa jimbo la Hai kwa tiketi ya
Chadema ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe alieleza
kuwa, walishindwa kuvumilia kuona ujio wa Dk. Shein akiingia Bungeni
hapo pamoja na Mh. Pandu Kificho ambaye alidai hivi sasa sio Spika wa
Baraza la Wawakilishi kwa kuwa Baraza hilo lilikwisha vunjwa.
Tumeshangaa kuona Pandu Kificho anaingia
kama Spika wa Baraza la Wawakilishi wakati Baraza limeshavunjwa,
tulishangaa kuona Dk. Shein anaingia kama Rais wa Zanzibar wakati huo
kipindi chake cha kukaa madarakani miaka mitano kimekwisha kikatiba,
alisema Mbowe.
Naye mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), Tundu Lissu alisisitiza kuwa wataendelea kuonesha msimamo wao
huku akimlalamikia Spika wa Bunge Mh. Job Ndugai kuwa anaendesha Bunge
hilo kibabe.
“Leo hii askari wenye uniform, mae-FFU
askari wa fujo wameingia ndani ya ukumbi wa Bunge. Sasa kwa wasiofahamu,
ukumbi wa Bunge katika nchi kama za kwetu na nchi zinazofuata utaratibu
kama wa kwetu, Ukumbi wa Bunge huwa haingii mtu yoyote asiyekuwa
Mbunge. Ndio maana ili Makamu wa Rais na wale wakubwawakubwa tuliokuwa
tunawapigia kelele? waingie, ilibidi tutengue kanuni ili kuwaruhusu
waingie”, alisema Tundu Lissu.
Mwenyekiti wa Wabunge wa Chama cha
Wananchi (CUF), Juma Hamad Omary alimtaja Maalim Seif Sharif Hamad kuwa
kiongozi anayepaswa kuigwa kwa kuwa aliwahi kukubali kushindwa mara
kadhaa licha ya mapungufu kuonekana na kwamba hata alipokuwa Makamu wa
Kwanza wa rais na kisha wawakilishi wa CCM kukataa asuhudhurie kwenye
sherehe za kufunga Baraza la Wawakilishi, aliamua kutohudhuria.
Chanzo: Dar24