Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imewagomea kulipa kodi bila adhabu baadhi ya
wamiliki wa makontena, ambayo yalitoroshwa kwenye bandari kavu bila
kulipiwa kodi.
Badala yake, TRA imewapelekea hati ya
malipo inayowataka wafanyabiashara hao, kuhakikisha wanalipa kodi hiyo
na adhabu ndani ya siku saba, la sivyo watafikishwa mahakamani kujibu
tuhuma hizo.
Hatua hiyo inatokana na baadhi ya
wamiliki wa makontena hayo, kuiomba TRA kuwasamehe kulipa adhabu
waliyopewa badala yake waruhusiwe tu kulipa kodi stahiki ya Serikali.
Jumla ya makontena 349 yalitoroshwa katika bandari kavu bila kulipa kodi na kuikosesha Seri kali mapato ya Sh bilioni 80.
Wafanyabiashara hao, pia wameomba
waruhusiwe kulipa kodi wanayotakiwa kulipa kidogo kidogo kwa madai kuwa
wengine hawana uwezo wa kulipa kiasi hicho cha fedha kutokana na
kutapeliwa na mawakala wao waliowatumia kwenda kulipa kodi hiyo.
Wakizungumza na wanahabari, baadhi ya
wafanyabiashara hao walisema agizo la Dk Magufuli alilotoa Desemba 3,
mwaka huu kuwa linawataka walipe kodi hiyo ndani ya siku saba.
Lakini wafanyabiashara walisema
nyaraka za malipo walizopelekewa na TRA, zimewataka kulipa kodi na faini
kwa pamoja wakati hizo siku saba alizotoa Dk Magufuli hazijamalizika.
Wafanyabiashara hao wanadai kuwa
walishalipa kodi hiyo kupitia kwa wakala wao, kama taratibu za TRA
zinavyowataka kuwatumia mawakala wa bandarini kulipa kodi, lakini kwa
bahati mbaya wakala huyo hakufikisha kodi hiyo serikalini.
Walidai kuwa walifuatilia nyaraka za kodi kwa wakala wetu, lakini akawa anawaambia wasubiri.
“Tunaomba hii adhabu tusamehewe,
kwani sio kosa letu ila tuko tayari kulipa kodi halali ya Serikali,
lakini wakala wetu ndiye katuingiza kwenye matatizo haya na yeye tayari
ameshatoroka,” aliongeza mfanyabiashara huyo.
Katika nyaraka za kodi ambazo TRA imewapelekea, kontena moja linatakiwa kulipiwa ushuru wa Sh milioni 40.5 ndani ya siku saba na adhabu ya Sh milioni 28.3. Hivyo jumla wanatakiwa kulipa Sh milioni 68.8 kama ushuru na adhabu.
Akizungumza na mwandishi kuhusu madai
hayo ya wafanyabiashara, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa
Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema adhabu walizoandikiwa
wafanyabiashara hizo, wanatakiwa kuzilipa pamoja na kodi stahiki ndani
ya siku saba.
Alisema wamewawekea adhabu hiyo
kutokana na kitendo chao cha kuiibia Serikali na kwa taratibu za nchi,
walitakiwa wawe mahabusu sasa hivi, lakini wametakiwa kulipa ushuru wa
Serikali wakati wakiwa nje; hivyo wanastahili kulipa kiasi hicho cha
fedha kama adhabu ya kukwepa kodi.
“Hawa walitakiwa kukamatwa na
kuwekwa ndani, walitoa kontena nje ya utaratibu, adhabu hiyo ni ya kutoa
makontena bila kulipa kodi,” alisema Kayombo. “Wakishindwa kulipa ndani ya muda huo tutawakamata tena na kuwafikisha mahakamani,” alieleza.
Kayombo alifafanua kuwa siku saba hizo
walizopewa wafanyabiashara hao ni kusamehewa kutoshitakiwa mahakamani
na sio kusamehewa kulipa adhabu wakati tayari walishakiuka taratibu.
Alisema wafanyabiashara hao, wachague
kulipa ndani ya siku saba wasishitakiwe au waache ili wakutane na rungu
la dola la kufikishwa mahakamani.
Alisema hadi sasa TRA imeshakusanya Sh
bilioni 9.4 kati ya Sh bilioni 80 zinazotakiwa kulipwa kutoka kwa
baadhi ya wafanyabiashara hao waliokwepa kodi.
CREDIT: MPEKUZI