* Awaonya Wakurugenzi, Maafisa elimu
SERIKALI imekwishatenga
kiasi cha sh. bilioni 137 kwa ajili ya kugharamia utoaji wa elimu ya
bure kuanzia Januari hadi Juni, mwakani.
Kauli hiyo imetolewa
jana jioni (Jumapili, Desemba 20, 2015) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa uwanja wa mikutano wa
Likangala wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
“Kazi ya utumbuaji
majipu imezaa matunda kwani tumeweza kupata fedha za kugahrimia elimu ya
bure ambayo iliahidiwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli wakati wa
kampeni. Fedha hiyo tunayo, na tumeshaanza kuisambaza kwa sababu
tunataka shule zikifunguliwa Januari, 2016 watoto waanze kufaidika,”
alisema huku akishangiliwa.
“Atakayezigusa fedha
hizi na kuzitumia vibaya ni lazima tutamtumbua tu! Tumeshawapa maelekezo
Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Maafisa Elimu wao na kuwaonya
kuhusu matumizi ya fedha hizo,” alisema.
“Hatuhitaji mwanafunzi
achangishwe hela ya mitihani, na zile shilingi 10,000/- kwa ajili ya
wanafunzi wanaosoma Sekondari nazo pia tutazipeleka. Na huu ni mpango wa
dharura ambao haukuwemo katika bajeti ya mwaka 2015/2016, kwa hiyo
tutalazimika kuziombea kibali,” alisema.
Waziri
Mkuu Majaliwa
alisema Serikali imekwishafanya hesabu za kubaini kiasi kinachohitajika
kwa ajili ya milo ya watoto shuleni kwa wale walioko bweni na wale wa
kutwa. Hesabu tunazo na tumebaini kuwa tutazimudu,” alisema huku
akishangiliwa.“Serikali ilitoa ahadi kwa wananchi na sisi tumedhamiria
kuzitekeleza. Tuliahidi elimu bure nasi tutaitekeleza,” alisema.
Naye Waziri wa Habari,
Utamaduni, Wasanii na Michezo, Bw. Nape Nnauye amewataka madiwani wa
jimbo la Ruangwa kuhakikisha wanamsaidia Waziri Mkuu Majaliwa kusimamia
kazi za jimboni ili aweze kuwa huru kutekeleza majukumu ya kitaifa.
“Madiwani wa jimbo hili
msaidieni Waziri Mkuu kusimamia shughuli za maendeleo ili wakati yeye
anaendelea kutekeleza majukumu ya kitaifa, ya jimbo naye yawe shwari.
Msaidieni kusimamia fedha za umma ziende kwenye miradi iliyokusudiwa ili
wakati akitumbua majipu huko kwingine na huku pia yasiote,” aliongeza.