Katibu Mkuu wa
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa. Elisante Ole Gabriel
akizungumza wakati wa mkutano baina yake na Naibu Waziri wa Habari, Utangazaji
na Utamaduni wa Serikali ya Jamhuri ya watu wa China Mhe. Tian Jin (kushoto)
jana jijini Dar es Salaam. Waziri huyo yupo nchini kwa ziara ya kikazi.
Baadhi ya
viongozi kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaaa na Michezo wakifuatilia
mkutano baina ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo
na Naibu Waziri wa ,Habari,Utangazaji na Utamaduni Mheshimiwa Tian Jin
jana jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Habari (MAELEZO) Bibi. Zamaradi Kawawa, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu
Tanzania Bibi. Joyce Fissoo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Taifa
(TBC1) Bw. Clement Mshana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Magazeti ya
Serikali (TSN) Bw. Gabriel Nderumaki.Picha zote na
Frank Shija, WHUSM.
China kuipiga jeki Tasnia ya Filamu nchini
Na: Frank Shijja, WHUSM
Serikali ya
Jamhuri ya Watu wa China yaonyesha nia ya kusaidia katika ukuajji wa sekta ya
Filamu nchini kwa kushirikiana na Bodi ya Filamu hapa nchini.Hayo
yamebainishwa jana na Naibu Waziri wa Habari, Utangazaji na Utamaduni wa
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China Tian Jin katika kikao baina yake na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Elisante Ole
Gabriel leo jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri
huyo amesema kuwa Serikali ya Watu wa China ipo tayari kushirikiana na Bodi ya
Filamu ya Tanzania ili kuimarisha ukuaji wa sekta ya Filamu hapa nchini kama
ilivyo nchini China.“Nitashirikiana
nanyi katika kuboresha tasnia ya Filamu katika hili nitaangalia namna ya
kuwezesha Filamu za Tanzania ziweze kuonyeshwa katika vituo vya Televisheni na
kwenye kumbi za sinema nchini kwetu” Alisema Tian Jin.
Aliongeza kuwa
sekta Filamu nchini China imekuwa kwa kasi kubwa ambapo kwa mwaka uzalishwa
takribani Filamu 650 zikiwa katika ubora na viwango vya hali ya juu na
kupelekea China kuwa nchi ya pili duniani katika ukuaji wa tasnia ya Filamu
ikitanguliwa na India.Kutokana na
ushirikiano uliopo Serikali ya Watu wa China imeahidi kuendelea kutoa
ushirikiano kwa dhati kabisa ili kuhakikisha sekta za Habari, Filamu na Sanaa
zinakua katika viwango bora zaidi.
Jin ameongeza
kuwa katika sekta ya Habari na Utangazaji Serikali yake imeahidi kuendeolea
kuvijengea uwezo vyombo vya habari vya Serikali ikiwemo TBC1 na Kampuni ya
Magazeti ya Serikali (TSN) ili vifanye kazi kwa weledi na ufanisi zaidi.
Kwa upande wake
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Elisante
Ole Gabriel ameiomba Serikali ya China kupitia Wizara yenye dhamana na sekta za
Habari, Utangazaji na Utamaduni kusaidia mambo matatu muhimu ambayo ni
kuendeleza na kuimarisha mpango wa kubadilishana uzoefu, kuwezeshwa kwa vifaa
bora na vya kisasa na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kukuza sekta za
Habari, Filamu na Utamaduni.
Elisante
aliongeza kuwa pamoja na ushirikiano mzuri uliopo baina ya nchi hizi mbili ni
vyema kuwekwe msukmo wa kusaidi hasa katika nyanja tatu muhimu ambazo alizitaja
kuwa ni; mpango wa kubadilshana uzoefu, uboreshwaji wa vifaa vya kufanyia kazi
pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa.Aidha aliongeza
kuwa ni vyema kukawa na utaratibu wa watu kujifunza lugha za pande mbili zenye
ushirikiano ili kuepuka matumizi ya wakalimani wakati wa mikutano na shughuli
zingine za kiutendaji.
Naye Katibu
Mtendaji wa Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo akitoa maoni ya juu ya hatua ya
Serikali ya Watu wa China kuvutiwa na sekta ya Filamu nchini alisema kuwa thamani
iliyoonyeshwa katika tasnia ya Filamu ni fursa ambayo watanzania tunapaswa
kuona faraja na nuru mbele yetu kwa nchi kubwa kama China kushiriki katika
kukuza tasnia hiyo hapa nchini hii itasaidia watanzania kupanua wigo wa kufanya
kazi za filamu kwa viwango na ufanisi wa hali ya juu.
Fissoo alisema
kuwa yeye kama Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini wamepokea kwa furaha hatua
hiyo na kuahidi kutoa ushirikiano kwa kila hatua ili kusukuma mbele gurudumu la
maendeleo ya tasnia ya Filamu nchini.Aliongeza kuwa
kwa kushirikiana na Serikali ya Watu wa China tasnia ya Filamu nchini itakuwa
kwa kasi na viwango hasa kutokana na mpango wa
kubadishishana uzoefu, matumizi ya teknolojia na vifaa vya kisasa.