Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Mpango (kushoto) akiongea na waandishi wa habari (hawamo pichani)jijini Dar es Salaam, kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali dhidi ya Benki ya Stanbic Tanzania kutokana na ushiriki wake katika kuwezesha mkopo wa Serikali wa Dola za Kimarekani Milioni 600 na Kulia kwake ni Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania(BOT) Bw. Lila Mkila.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Mpango (katikati) akitoa tamko kwa waandishi wa habari (hawamo pichani) jijini Dar es Salaam, kuhusiana na kusudio la kuitoza Benki ya Stanbic faini ya shilingi bilioni 3. Kulia kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dkt. Servicius Likwelile na Kushoto kwake ni Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Bw. Lila Mkila.
………………
Utangulizi
Mwezi Julai 2013, Benki Kuu ya Tanzania kupitia ufuatiliaji wa kawaida wa shughuli za mabenki iligundua matatizo yaliyohusiana na hasara itokanayo na mikopo na pia kuacha na kuondolewa kazini kwa viongozi waandamizi wa Stanbic Bank Tanzania Limited (Stanbic) katika muda mfupi. Kutokana na hilo, Benki Kuu iliamua kufanya ukaguzi wa kulenga (Targeted Examination) katika benki hiyo. Ukaguzi huo ni kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa Benki Kuu chini ya Kifungu 47 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 na Kifungu 31 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
Matokeo ya Ukaguzi wa Benki Kuu
Katika ukaguzi huo, wakaguzi wa Benki Kuu, pamoja na mambo mengine walibaini miamala ya kutia shaka iliyohusu malipo kwa kampuni ya kitanzania ya Enterprise Growth Market Advisors (EGMA). Kampuni ya EGMA ilihusika katika uwezeshaji wa upatikanaji wa Mkopo kwa Serikali ya Tanzania ambapo Standard Bank Plc (ambayo kwa sasa inajulikana kama ICBC Standard Bank) na Stanbic Bank Tanzania Limited kwa pamoja walikuwa “Mwezeshaji Mkuu” (Lead Arranger). Malipo hayo kwa kampuni ya EGMA yalikuwa yamefanyika kinyume na taratibu za kibenki na yalihusisha uongozi wa benki ya Stanbic. Jumla ya malipo yalikuwa ni kiasi cha dola za kimarekani milioni 6, na zililipwa katika akaunti ya EGMA na kutolewa kwa muda mfupi kwa njia ya fedha taslimu (cash) ambayo ni nje ya taratibu za kibenki.
Taarifa ya ukaguzi huo iliwasilishwa kwa benki ya Stanbic kwa mujibu wa taratibu, na Benki Kuu iliiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo kuchukua hatua stahiki za kurekebisha kasoro zilizoonekana. Aidha, benki ya Stanbic iliagizwa kutoa taarifa kwa Kitengo cha Financial Intelligence Unit (FIU) kilichopo Wizara ya Fedha na Mipango kuhusiana na miamala hiyo yenye mashaka katika akaunti ya EGMA kama Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu ya mwaka 2006 (The Anti-Money Laundering Act, 2006) inavyoelekeza. Benki ya Stanbic ilitekeleza maagizo na kutoa taarifa FIU kuhusu miamala inayotiliwa shaka.