Na Nyakongo Manyama- MAELEZO.
Wizara ya Nishati na Madini imekanusha habari iliyopotosha umma
kuhusu mradi wa umeme wa Kinyerezi II kuwa bado haujaanza na gharama
zilizoandikwa si za kweli.
Wizara hiyo imekanusha habari hiyo, iliyoandikwa katika gazeti la
Mtanzania la leo Januari 14, mwaka huu toleo namba 8063, lenye kichwa
cha habari “ Harufu ya Jibu Mradi wa Umeme.”
Habari hiyo ambayo ilieleza kwamba mradi huo ulizinduliwa na Rais
Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Mhe. Dkt.Jakaya Kikwete uligharimu
Sh. trilioni 1.6 na kwamba fedha za ujenzi wa mradi huo zimetokana ubia
kati ya Serikali ya Tanzania na Japan,ambapo Serikali ya Tanzania
itakuwa na hisa ya asilimia 40 na kampuni ya SUMITOMO ya Japan asilimia
60.
Aidha habari hiyo ilidai kuwa Serikali inachangia fedha za ndani
kwa asilimia 12 na zilizobaki zikiwa na mkopo kutoka benki ya Japan na
kwamba gharama za mradi huo ziko juu ikilinganishwa miradi mingine
akitolea mfano Kampuni ya TALLAWARA Power Station ya nchini Australia
anayodai ilitaka kujenga mradi huo kwa dola za Marekani milioni 350.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mawasiliano Serikali wa wizara hiyo,
Badra Masoud alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu habari
hiyo katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam.
“Serikali ya Tanzania iliingia makubaliano na Serikali ya Japan ya
mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 292 kwa ajili ya
kutekeleza mradi wa kuzalisha umeme wa Megawati 240 utakaojengwa na
kampuni ya SUMITOMO kama mkandarasi wa “EPC contractor” na sio kama mbia
wa Serikali yaTanzania kama ilivyodaiwa.
“Mradi huo unamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 kupitia TANESCO na hakuna mwekezaji mwingine katika mradi huo.
Hivyo si kweli kwamba Serikali ya Tanzania na kampuni ya SUMITOMO
zinawekeza kwa ubia wa asilimia 40 (kwa Serikali ya Tanzania) na
asilimia 60 kwa SUMITOMO. Kwa maana hiyo hatutauziwa umeme
utakaozalishwa na mradi huu kwani ni mali yetu na hakuna gharama yoyote
ya ziada kama alivyodai mwandishi wa habari hiyo,” alisema Badra.
Aidha Badra alisema mwandishi huyo alidai kwamba mradi huo
ulizinduliwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya
Kikwete, wakati ni kwamba mradi huo haujazinduliwa bado na sasa upo
katika maandalizi ya kuwekwa katika jiwe la msingi.
Akizungumzia kuhusu gharama za mradi huo, alieleza kuwa
unatekelezwa kwa dola za Marekani milioni 344 sawa na Sh. bilioni 740
zikiwa ni mkopo wa masharti nafuu wa asilimia 85 sawa na dola za
Marekani 292 na mchango wa Serikali ya Tanzania kwa asilimia 15 sawa na
dola za Marekani milioni 52.( na sio asilimia 12 kama ilivyodaiwa na
mwandishi huyo).
“Mwandishi wa habari hii amejaribu kufananisha uwekezaji huu na
uwekezaji wa TALLAWARA Power Station ya Australia na kudai kwamba
gharama yake ingekuwa ndogo kuliko gharama ya mradi huu. Taarifa hii
haina ukweli wowote kwa sababu gharama ya dola milioni 344
zinazotarajiwa kutumika mkatika mradi huu iko chini kuliko dola milioni
350anazodai mwandishi kwamba zingetumiwa na kampuni TALLAWARA.
“Aidha, kampuni ya TALLAWARA haijawahi kuomba au kuonesha nia ya
kuwekeza katika mradi wowote wa kufua mradi wa umeme nchini. Pia ni
muhimu ifahamike kwamba makubaliano ya mkopo huu yalikuwa yanakwenda
sambasamba na utekelezaji wa mradi wenyewe (EPC with Financing).
Badra aliongeza kwamba pamoja na kwamba gharama za uwekezaji wa
mradi huo wa kwanza wa aina ya “Combined Cycle” nchini zinawiana na
gharama za miradi mingine ya aina hiyo duniani, gharama za uwekezaji
zinaweza kutofautiana kutegemeana na mazingira ya nchi na nchi,
teknolojia iliyotumika na aina ya mitambo.
Hivyo sio suala la kulinganisha gharama ya mradi mmoja na mwingine .
Wizara hiyo imeshauri waandishi wa habari kufuata miiko na maadili
ya uandishi wa habari kwa kuandika habari zenye ukweli na sahihi na
zilizozingatia pande zote mbili kwa kuwa ipo na tayari kujibu maswali ya
waandishi wakati wowote.