Chama
cha ACT-Wazalendo kimesema kimeshtushwa na tuhuma dhidi ya kiongozi
wake wa chama, Zitto Kabwe kwamba ana miliki mali za kifisadi pamoja na
kuhusishwa na ununuzi wa ardhi maeneo ya Kigamboni uliofanywa na NSSF
kwa bei ya milioni 800 kwa ekari moja, wakati bei halisi ni milioni 25
na kwamba kitendo hicho kimeitia hasara serikali .
Tuhuma hizo zilitolewa jana na Msemaji
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Christopher Ole Sendeka, ambapo alivitaka
vyombo vya uchunguzi kufanya uchunguzi katika shirika hilo ili kubaini
waliohusika kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria, huku akimhusisha
Zitto katika uchunguzi huo.
Ole Sendeka alitaka akaunti za benki
za Zitto pamoja na maisha yake binafsi kuchunguzwa kama yana uhalisia na
kipato chake halali.
Tuhuma hizo zimekiibua chama cha ACT,
ambapo leo Katibu wa Bunge na Serikali za Mitaa ACT, Habibu Mchange
amevitaka vyombo vya uchunguzi haraka iwezekanavyo kuchunguza mali,
madeni, akaunti zote za benki pamoja na mfumo wa maisha ya Zitto.
“ACT imeshtushwa na tuhuma, kashfa,
porojo na matusi mbalimbali yaliyotolewa jana na Ole sendeka dhidi ya
kiongozi wa chama chetu,” amesema.
Amesema kuwa, katiba ya chama hicho
huwataka viongozi wote kuweka hadharani matamko ya mali zao na madeni na
kwamba Zitto alitekeleza matakwa hayo ya kisheria hivyo mali na madeni
yake yako hadharani na mtandaoni.
“Tunaamini kama kuna kiongozi ambaye mali, madeni, maslahi, na akaunti zake viko wazi basi ni ndugu Zitto,” amesema.
Aidha, Mchange amedai kuwa,
kilichomsukuma Sendeka kutoa tuhuma hizo kwa Zitto ni harakati zake za
kuupinga muswada mpya wa habari.
“Tuhuma za ole sendeka kuna kitu
nyuma yake, jitihada za zito za kupambana na mswada wa habari ndizo
zilizomuibua, sababu wanataka upitishwe ili kuviua vyombo vya habari,” amesema.
Amesema ACT itaendelea kuisimamia serikali katika mambo ya bungeni kama anavyofanya mbunge na kiongozi wao wa chama.