Rais wa Colombia Juan Manuel Santos
ameshinda Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 2016 licha ya kuvunjika kwa
mkataba wake wa kusitisha vita na waasi wa Farc nchini humo.
Rais
Santos aligongwa vichwa vya habari baada ya kufanikiwa kupata
makubaliano ya amani na waasi hao jambo ambalo lilifikisha kikomo vita
vilivyodumu kwa karibu miaka hamsini.Mkataba huo ulitiwa saini na Bw Santos na kiongozi wa waasi hao kamanda Rodrigo Londono, anayejulikana vyema kwa jina Timochenko mjini Cartagena tarehe 27 Septemba.
"Colombia inasherehekea, ulimwengu unasherehekea kwa sasa kuna vita vimemalizika duniani," alisema wakati huo.
"Tutatimiza malengo yote, tutazidi nguvu changamoto zote na kugeuza nchi hii kuwa taifa ambalo tumekuwa tukitaka liwe, taifa la amani."
Watu 260,000 waliuawa kwenye vita hivyo na wengine milioni sita kuachwa bila makao.
Mapatano hayo na kundi la waasi la Farc yalikataliwa na raia katika kura ya maoni iliyoandaliwa Oktoba 2.
Wakosoaji wanasema kuwa mkataba huo wa amani unawapa waasi wa Farc fursa ya kukwepa haki kwa makosa waliyofanya.
Lakini rais Santos kwa upande wake anasema kuwa hayo ndiyo mapatano bora zaidi yanayoweza kufanywa kwa niaba ya Colombia.
Baadhi ya wanachama wa FARC, pamoja na maafisa wa kijeshi na polisi walipangiwa kufikishwa mbele ya mahakama maalumu kujibu mashtaka kwa makosa ambayo wametekeleza katika vita nchini humo chini ya mkataba huo.
Kundi la Farc, ambalo lilianza kama wanamgambo wa Chama cha Kikomunisti mwaka 1964, linatarajiwa kuacha vita na kuingia katika siasa za amani.