Maafisa nchini Afghanistan wanasema
wanamgambo wa Taliban wamepiga hatua kubwa katika juhudi zao za kuteka
mji wa Kunduz ambao unapatikana kaskazini mwa taifa hilo.
Pia, wamepata mafanikio katika mji wa Helmand maeneo ya kusini.Mapigano makali yanaendelea katika mji wa Kunduz baada ya wanamgambo hao kuanzisha operesheni kubwa ya kutaka kuuteka usiku.
Msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid amesema wapiganaji wa kundi hilo wameteka maeneo kadha muhimu mjini humo.
"Operesheni kubwa ilianza katika mji wa Kunduz kutoka pande nne mapema asubuhi hii," Bw Mujahid alisema kupitia Twitter.
Mji huo ulitekwa na wanamgambo hao wa Taliban Septemba mwaka jana lakini ukakombolewa na wanajeshi wa serikali baada ya siku nne.
Mjini Helmand, taarifa zinasema wapiganaji wa Taliban wameteka maeneo muhimu ya Nawa, ambayo ni kama lango la kuingia mji mkuu huo wa mkoa wa Lashkar Gah.
Wachanganuzi wanasema serikali inakabiliwa na shinikizo kubwa kuchukua hatua na kudhibiti tena maeneo hayo.