ASKOFU wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu ametoa wito kwa jamii kuwekeza zaidi katika elimu kwa kuwasomesha watoto wa kike na kuacha mila na desturi mbaya ya kuwaozesha kwa tamaa ya ng’ombe.
Akiongea na wazazi na walezi katika mahafali ya 18 ya kidato cha nne ya shule ya sekondari ya Don Bosco iliyopo Didia jimboni Shinyanga, Askofu Sangu ameitaka jamii kuwekeza zaidi kwenye elimu kwa kutoa upendeleo kwa wasichana kwa sababu ukimwelimisha mtoto wa kike umeelimisha taifa.
Askofu Sangu amesema familia bora hutokana na mama aliyeelimika na kuitaka jamii kuacha mila na desturi mbaya zilizopitwa na wakati za kuwaozesha watoto wa kike katika umri mdogo kwa ajili ya tamaa ya mali na ng’ombe.
Amesema katika ukanda wa mkoa wa Shinyanga unaokabiliwa na changamoto ya mauaji ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi ( albino ) kwa imani za kishirikina kutokana na ujinga na tamaa ya mali jamii inatakiwa kupiga vita vitendo hivyo kwa kuwekeza kwenye elimu inayowajenga watu kwenye uelewa.
“ Ujinga ni mbaya sana hasa kwa nyakati hizi ndiyo unaosababisha baadhi ya watu kuwaua wenzao kwa imani za kishirikina, huwezi ukamtafuta Mungu kwa ujinga, tunahitaji elimu ya ukombozi itakayotusaidia kumjua Mungu katika maisha yetu,” amesema Askofu Sangu.
Askofu Sangu amewaasa vijana wanaohitimu elimu yao kuishi kwa matendo mema na wawe mitume wa upendo kwa wazazi na walezi wao na mahala popote watakapoishi na wawe chimbuko la maendeleo ya kiroho na kimwili huku akiwataka wasibweteke na elimu hiyo bali wajiendeleze zaidi.
Naye Mkuu wa shule ya Sekondari ya Don Bosco yenye wanafunzi mchanganyiko wa kiume na kike Padri Richard Mtui katika taarifa yake amesema jumla ya wanafunzi 176 wamehitimu kidato cha nne na kuwataka kutumia malezi na elimu waliyoipata vizuri katika kupambana na changamoto mbalimbali katika maisha yao.
Kwa upande wake Padri Mathias Isaka amewataka wazazi na walezi kuendelea kuwasaidia watoto hao katika kuwajenga kiroho na kimwili juu ya kuwaasa, kuwakemea, kuwaonya kwa sababu dunia ya sasa vijana wanakabiliwa na changamoto nyingi ili wasiweze kujiingiza katika makundi maovu yenye tabia mbaya miongoni mwa jamii