“Acheni kupokea Ekaristi Takatifu ili muonekane kuwa mmekomunika, ili hali mnajua kuwa hamustahili, kama haujaenda kwenye kitubio halafu ukapokea Ekaristi Takatifu, unakuwa umeiba sakramenti”.
Hayo yameelezwa na Makamu wa Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro Padri Patrick Kung’alo alipokuwa akitoa sakramenti ya komunyo ya kwanza kwa vijana zaidi ya 30 pamoja na kuweka jiwe la msingi kwenye kanisa la Kigango cha Kristo Mfalme Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli iliyopo Kihonda Magorofani linalotarajia kujengwa karibuni.
Padri Kung’alo amesema kuwa asilimia kubwa ya waamini wamekuwa wakikomunika kama “fasheni” ili aonekane aidha kwa mavazi aliyovaa na muonekano wake kwa ujumla huku wakisahau kuwa Ekaristi Takatifu siyo ya kufanyia mchezo.
“Wengi tunawaona wanakomunika ili waonekane walivyovaa na kupendeza au kwa kuwa wanaona kuwa kubaki peke yao kwenye viti watafikiriwa vibaya, matokeo yake wanaenda kukomunika hali ya kuwa wanajua matendo hayo hayastahili.” amesema.
Ameongeza kuwa waamini wanapaswa watafakari kabla ya kwenda kukomunika ama sivyo sakramenti hiyo itawapeleka pabaya, kwa kuwa wanapoungamisha unakuta wanaoungama hawafiki hata 30 hawafiki lakini kwenye kukomonika wanakuwa wengi.
“Unakuta tunaungamisha waamini hawafiki 30 lakini kwenye kukomonika unajikuta unamaliza yale makombe hata matatu sasa unajiuliza hawa watu wamefanya wapi kitubio au ndio wapo safi hawajatenda dhambi?,” amesema Padri Kung’alo.
Ameongeza kuwa kama kweli waamini hawatendi dhambi kwa nini unakuta mtu na jirani yake hawasalimiani kufikia kuapizana vibaya , ndoa zinafuka moshi, umbea, masimango mawazo mabaya na mengine mengi ambayo ni dhambi lakini unakuta muumini anafukia hayo yote pasipo kutafakari kwa hayo yote kama anastahili kukomunika au la.
“Tusicheze na Ekaristi Takatifu, kama utaipokea ukiwa katika hali ambayo inatakiwa kwa kufanya kitubio ndipo upokee, itakupa uzima wa milele lakini kama na wewe ni mmoja wa wale wanaopokea kwa fasheni itakupeleka pabaya. Hivyo tubu na uhakikishe uko safi na usikomunike kwa kuwa unahisi utasemwa kwa nini haujakomunika, hali ya kuwa unajua moyoni unatakiwa utubu ndipo ukomunike,” amesema Padri Kung’alo.