Serikali
inatarajia kupiga marufuku utengenezaji na uingizaji wa pombe za bei rahisi maarufu
kama “Viroba” Nchini, ndani ya miezi mitatu ijayo.
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamisi
Kigwangalla ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu hoja za
wabunge waliokuwa wakilalamikia kilevi
hicho kinavyopunguza nguvu kazi ya Taifa, wakati wa uwasilishwaji wa taarifa za
kamati ya kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi pamoja na Huduma na Maendeleo ya
Jamii kwa mwaka 2016/17.
Dkt.
Kigwangalla amesema kuwa baada ya miezi mitatu kilevi hicho kitapigwa marufuku
kutengenezwa au kuingizwa nchini pamoja na kuziba mianya yote ya uingizaji wa
kilevi hicho ambacho kimekuwa kikitumiwa na vijana wengi, hivyo kuharibu nguvu
kazi ya Taifa.
Kwa
upande wake Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini Esther Matiko amesema kwamba pombe
hiyo inasababisha vifo vya vijana wengi nchini ambao ndio tegemeo kubwa na
nguvu kazi ya Taifa.
“Katika
kipindi hiki kifupi cha likizo yangu, nilikuwa jimboni kwangu na tumezika
vijana wanne ambao wamefariki kutokana na matumizi ya viroba. Hivyo wananchi wa
jimbo langu wameniagiza kuja kulieleza Bunge athari za pombe hiyo ili tuweze
kujadili na kuona namna gani ya kuliokoa
Taifa hasa vijana kutoka katika janga hilo,” alifafanua Matiko.
Akiwasilisha
taarifa ya Kamati, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile
amesema kuwa Kamati imebaini uwepo wa uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya pombe
hizo na kuongezeka kwa tabia hatarishi zinazochangia ongezeko la vijana katika
matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha
amesema kuwa hali hiyo inaathiri ufanisi wa nguvu kazi ya Taifa kutokana na
madhara ya matumizi ya dawa za kulevya. Hivyo Kamati imeishauri Serikali kufungia
kabisa uzalishaji na uuzwaji wa pombe hizo za viroba ili kulinusuru Taifa.