Msanii wa muziki wa kughani
nchini Tanzania, Mrisho Mpoto amesikitishwa na kifo cha Mzee Francis
Kanyasu aliyechora Nembo ya Taifa na kusema anatamani siku zirudi nyuma
ili aweze kuongea naye tena. Mpoto
amefunguka hayo kupitia ukurasa wake wa instagram kwa kudai Mzee huyo
alishawahi kumsaidia kumpa wazo la kufanya video ya wimbo wake wa 'Njoo
ichukue'.
"Hii ni taarifa ya
kunisikitisha sana kwenye maisha yangu ya muziki, nakumbuka kabla ya
kutoa wimbo wa 'Sizonje' nyuma yake nilitoa 'Njoo nichukue' huyu Mzee
alikuja ofisini kwangu kuniambia maneno mazito sana kwamba anapenda kazi
yangu na alinitabiria mambo mengi mazuri kwenye safari yangu ya maisha
nanukuu YACHUKULIE MANENO HAYA NI YA CHIZI KAONGEA" aliandika Mpoto.
Aidha Mpoto aliendelea kusema kuwa "Ombi
lake lilikuwa moja tu alitamani kufanya kazi na mimi, ofisi nzima
ikamchukulia kama mzee aliyechanganyikiwa wakataka kumfukuza, mlinzi
wetu wa ofisi akasema msimpuuze mpeni nafasi, tulipompa nafasi ndiyo
akatoa wazo la video ya wimbo wa 'Njoo uichukue' iweje, na akasema yule
mzee Mshuba kikongwe muuza bangi ataigiza yeye mwenyewe tulicheka Sana
maana wazo lake lilikua zuri na liliungwa mkono na 'Director' Adamu
Juma"
Pamoja na hayo Mpoto amesema baada ya kupata taarifa ya kifo ndipo alipokuja kugundua kuwa Mzee Francis anamfahamu vizuri.
"Baada ya kuangalia kwa
makini kumbe ndiyo yule mzee aliyefariki leo mchora Nembo ya Taifa,
natamani siku zirudi nyuma niongee naye tena, roho imeniuma sana kwa
kweli sijui hata nifanye, nini kibaya zaidi baada ya 'shooting'
alitutoroka hata hatukujua tutampataje".alisisitiza Mpoto