Joseph Kasheku, Mbunge wa Geita
Mbunge wa Geita (CCM), Joseph
Kasheku Musukuma amesema hawezi kumsifia hata kidogo Prof. Jumanne
Maghembe, Waziri wa Maliasili na Utalii kwani yeye na watu wake wa
Wizara wanafanya mambo ya ajabu hasa kwa watu wa Kanda ya Ziwa.
Musukuma
anasema watu wa Wizara ya Maliasili wamekuwa wakiuza ng'ombe za watu
jamii ya wasukuma na kuzipiga mnada kwa dili kwa lengo la kujinufaisha
wenyewe, hivyo mbunge huyo amesema wasukuma wameamua kuwa wataziroga
ng'ombe zote ili wanaokula ngo'mbe hizo Dar es Salaam wavimbe matumbo.
"Napata shida sana kujiuliza
labda sisi watu wa kanda ya ziwa labda tulikuja kwa bahati mbaya
Tanzania hii, mbona yanayofanyika Kanda ya Ziwa hayafanyiki Kanda ya
Kaskazini wakati nao wana mapori, Waziri ametoa siku tatu tukamatiwe
ng'ombe kwa kisingizio kwamba ni ng'ombe za Wanyarwanda wakati huo huo
watumishi wake wanaowaingiza Wanyarwanda wanawaambia toeni ng'ombe,
mnaenda kukamata ng'ombe za Wasukuma halafu unazipiga mnada na mnada
wenyewe unavyopigwa ni wa dili" alisisitiza Musukuma
Mbunge huyo aliendelea kuelezea namna watu wa Wizara ya Maliasili wanavyofanya minada hiyo huku wakiwaumiza wafugaji
"Yaani ng'ombe 600 unaambiwa
ulete milioni tatu halafu wanatoa watu wao wa Ubungo sasa hapo
nikupongeze kwa sababu gani? Tunajua mipango inayoendelea kwenye wizara
yako na niliwapigia kabisa watumishi wako, wananiambia mliipenda wenyewe
kwa kauli yake kama Mwenyekiti wa Chama kesho yake akapiga ng'ombe za
watu mnada yaani ng'ombe 500 zinauzwa milioni tatu" alisema Musukuma
Joseph Msukuma aliendelea na msimamo wake
"Nataka nikwambie sisi
Wasukuma sasa tumeamua na ninazungumza uelewe tutaziroga hizo ng'ombe
mtavimba matumbo mnaozila huko Dar es Salaam, haiwezekani kwanini
wanunuzi watoke Dar es Salaam peke yake yaani leo siku ya mnada watu
wametoka na malori Pugu wamejuaje kama wanakuja kushinda kwenye minada.
Mnatukamatia ng'ombe hivi hii serikali imekosa sehemu ya kukusanya hela
mpaka mkanyang'anye ng'ombe za wafugaji haiwezekani Mh. Maghembe"
source: EATV