Taarifa ya pili ya wachumi
na wanasheria iliyofanya uchunguzi wa madini yaliyo kwenye makontena
yenye mchanga wa madini iliyoundwa na Rais Joseph Magufuli, imebaini
kuwa kampuni ya ACACIA Mining Plc haina kibali na inafanya kazi kinyume
cha sheria.
Prof.
Osoro amesema kwamba Kamati yake imebaini kuwa Acacia haina uhalali wa
kufanya shughuli zake hapa nchini na imetenda makosa yakiwemo
kujipatia mali kwa udanganyifu, uhujumu uchumi, jinai na kuitia hasara
taifa.
Aidha Kamati ya Prof. Osoro imebaini
kwamba Makinikia yaliyouzwa nje ya nchi hayakuwa makinikia hasa, bali
yalikuwa ni madini mbalimbali huku ikiongeza kwamba katika mikataba ya
uuzwaji wa makinikia hayo, serikali haikuwa sehemu ya mikataba hiyo.
Prof. Osoro ameongeza kwamba jumla ya
mapato yote ambayo serikali imepoteza ni Tsh. trilion 68.6 sawa na
bajeti ya miaka miwili ya nchi kodi ya mapato ambayo taifa imepoteza ni
Tsh. tril 55.07, mrahaba tril 11, bandari tril 1.6. na kwamba jumla ya
thamani ya madini kwenye makontena yote 44,277 tangu mwaka 1998 ni Tsh.
tril 132.56.
Mwenyekiti wa Kamati ya Wachumi na Wanasheria ,Pro. Nehemia Osoro.
Pamoja na hayo imebainika kuwa
uongezwaji wa leseni kinyume cha sheria ambapo imedaiwa kuwa aliyekuwa
Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja na Sospeter Muhongo ndio
waliohusika na uongezaji wa muda kwenye uchimbaji wa madini.
Kamati hiyo imetoa mapendekezo
mbalimbali ikiwepo kuchukua sheria juu ya kampuni ya ACACIA iliyopo
nchini kinyume cha sheria kupitia msajili wa makampuni ikiwa ni pamoja
na Mawaziri wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine juu ya mikataba
ya uchimbaji madini huku ikiitaka Serikali iwe inafanya ukaguzi wa mara
kwa mara kwenye makampuni ya madini.