MY ADVERT EA SHOWBIZ

MY ADVERT EA SHOWBIZ

SIX OFFICE SOLUTION

MOCHRISPO

DARDY FASHION

Jun 12, 2017

Rais Magufuli awachimba mkwara wabunge

Rais Dkt. John Pombe Magufuli
Rais Dkt. John Pombe Magufuli leo amewachimba mkwara baadhi ya wabunge ambao huwa wanakazi ya kuropoka bungeni na kusema anawasubiri waropoke tena nje ya bunge ili adili nao vizuri kwani wamekuwa wakirudisha watu nyuma katika vita ya uchumi. 
Magufuli amesema hayo leo wakati akipokea ripoti ya pili iliyounda kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa madini kwenye makontena ya mchanga ambayo yanafahamika kama Makinikia, ambapo Rais ameahidi kuwa sheria zote za madini zinapaswa kupitiwa tena na kurekebishwa na bunge ili ziweze kuleta tija kwa Watanzania.
"Mhe. Spika Job Ndugai nitakuletea mizigo hii bungeni, lakini kwa wale wanaoropoka bungeni naona unaenda vizuri nenda na mwendo huo huo, maana wakiwa kule wanaweza kutukana wanalindwa na kinga ya bunge, ila ukiwatimua mwezi mzima wataropoka nje ya bunge, mimi nitadili nao vizuri. Siwatishi bali nawaambia ukweli huwezi kuwa unamrudisha watu nyuma kwenye vita hii, kama huna la kusema ni bora ukae kimya" alisema Rais Magufuli 
Mbali na hilo Rais Magufuli alikubaliana na mapendekezo yote 20 ambayo yameletwa na Kamati hiyo maalum chini Mwenyekiti Prof. Nehemiah Eliachim Osoro ikiwa ni pamoja na baadhi ya Mawaziri pamoja na viongozi wote waliohusika katika kusaini mikataba hiyo kutafutwa popote walipo na kuhojiwa na vyombo vya dola.
"Wahusika wote waliotajwa kwenye ripoti hii vyombo vya dola viwahoji na kujua ukweli juu ya jambo hili, hata kama wapo serikalini au wapo wanafanya biashara zao wahijiwe tu, maana wengine wamekuwa wafanyabiashara wakubwa kumbe wanatumia pesa zetu Watanzania ili kama hizo pesa zetu tuzichukue tu" alisisitiza Magufuli 
Rais Magufuli alikwenda mbali zaidi na kusema Tanzania kuna watu wanakosa madawa katika hospitali, huku akisema watu wengine wanakosa pembejeo mashambani kwa kuwa nchi ni masikini ili hali nchi ina utajiri mkubwa, ambao umekuwa ukitumika vibaya kutokana na tamaa za viongozi ambao siyo wazalendo, viongozi ambao hawajali maslahi ya Watanzania zaidi ya kuangalia maisha yao tu.
Katika hatua nyingine Spika wa Bunge Job Ndugai amekiri kuwa wao kama Bunge wapo tayari kupitia sheria zote zitakazokuja bungeni kwa umakini zaidi ili kuweza kurekebisha mikataba hiyo mibovu iliyoliingizia taifa hasara kubwa.