Hayawi
hayawi hatimae yamekuwa baada ya Kimya cha muda mrefu tangua Uwanja Mkongwe wa
Nyamagana ulioko Mkoani Mwanza kuingizwa katika orodha ya Viwanja vya
Shirikisho la Soka Duniani FIFA ili kuwekewa nyasi badia.
Baada ya Tathmini ya Muda mrefu katika Uwanja huo, hatimae
Ukarabati wa kuuwekea nyasi za bandia Uwanja wa Nyamagana Umeanza siku ya
jana
chini ya Kampuni ya Ujenzi ya Jasco ambayo imepewa tenda ya ukarabati huo.
Ili kufanikisha zoezi hilo la Uwekaji wa nyasi bandia katika
Uwanja huo wa Nyamagana, FIFA ilitoa kiasi cha dola za Marekani 500,000 ambapo Manispaa ya Jiji la Mwanza ambao ndiyo
wamiliki wa uwanja huo, imechangia kiasi cha dola 118,000 (Sh milioni 295) kama
mchango wake kwa ajili ya zoezi hilo ambalo linatarajiwa kugharimu dola 618,000
(Sh milioni 988).
Uwanja wa
Nyamagana utakuwa ni uwanja wa nne kuwekewa nyasi hizo za bandia hapa nchini
ambapo tayari viwanja vya Uhuru na Karume vya jijini Dar es Salaam na Migombani
cha Zanzibar vimewekewa nyasi hizo huku Uwanja wa Kaitaba Mkoani Kagera nao
ukiwa ni Miongoni mwa Uwanja ulio katika orodha ya kuwekewa nyasi bandia na
hivyo kuongeza idadi ya viwanja vyenye nyasi bandia hapa nchini.
“Hii ni
nafasi nzuri kwa wana Mwanza kuhakikisha mchezo wa soka unarudi kwenye nafasi
yake kwa kasi kama ilivyokuwa siku za nyuma nami niliahidi nilipofika mkoani
hapa kuwa nitahakikisha michezo inakuwa kwenye nafasi nzuri.” Hiyo ilikuwa ni
sehemu ya hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Evarist Ndikilo wakati
akitoa taarifa kwa wanahabari Mkoani Mwanza Miezi kadhaa iliyopita juu ya
Ukarabati wa Uwanja huo.
Chama cha
Soka Mkoani Mwanza MZFA kupitia kwa Mwenyekiti wake Jackson Manji Songora
kimefurahishwa na Ukarabati wa Uwanja huo ambao unaonekana utaweza kuongeza
chachu ya Kimichezo katika Mkoa wa Mwanza licha ya Mkoa huo kutokuwa na timu
inayocheza ligi kuu Msimu huu baada ya Timu tegemewa za Toto African Fc na Pamba
Fc juhudi zao za kurejea ligi kuu kutozaa matunda.