Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Manispaa
ya Ilala imevuka lengo la kutoa chanjo ya ugonjwa wa Surua na Rubella
kwa watu 468,297 ambapo awali lengo lao lilikuwa kutoa chanjo hiyo kwa
watu 445,801 wakati wa wiki ya kutoa chanjo hiyo nchini.
Hayo
yamesemwa na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Ilala Dkt. Willy
Sangu leo jijini Dar es salaam alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya
zoezi la chanjo hiyo linalofanyika nchi nzima.
Dkt.
Sangu alisema kuwa zoezi la kutoa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Surua na
Rubella linaendelea vizuri katika Manispaa ya Ilala kama ilivyopangwa
ambapo linafanyika kwa muda wa wiki moja katika kote nchini. “Ninawaomba
watu wote ambao hawajajitokeza kupata chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Surua
na Rubella, wafike kwenye vituo vya kutolea chanjo hiyo ili kuokoa
maisha ya watoto, akina mama wajawazito, akiba baba na vijana” alisema
Dkt. Sangu.
Dkt.
Sangu alisema kuwa idadi ya watu walioitikia wito wa kupata chanjo hiyo
imekuwa kubwa katika Manispaa ya Ilala suala ambalo linawapa faraja
ambapo watu wa rika zote wamejitokeza kupata huduma.
Ili
kutoa huduma ya chanjo kwa wakati kulingana na ratiba, Dkt. Sangu
amesema kuwa imewalazimu kuongeza vituo 30 ambapo timu ya wahudumu
kutoka kwenye vituo mama inatoka ili kuwafuata wananchi waliko.
Awali Manispaa ya Ilala ilitenga vituo 236 vya kutoa chanjo hiyo kwa wananchi ndani ya Manispaa hiyo.
Dkt. Sangu amesema kuwa mafanikio idadi kubwa hiyo ya mwitikio wa watu kupata
chanjo katika manispaa ya Ilala yanatokana na sifa ya kuwa katikati ya
jiji ambapo watu wengi hupata huduma mbalimbali za kijamii.
Kwa
upande wake Afisa Muuguzi Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo Ilala Queen
Lutufyo amesema kuwa mwitikio wa watu kuja kupata chanjo ni mzuri na
hawajakosa wateja muda wote wakati wa kutoa huduma hiyo kituoni hapo.
Aidha,
katika zoezi la kutoa chanjo hiyo magonjwa ya Surua na Rubella wahudumu
pia wanatoa dawa za magonjwa ya matende, mabusha, minyoo na matone ya
vitamin ‘A’.
Muda
wa kutoa huduma hiyo ya chanjo vituoni ni kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa
kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni licha ya kwanba wakati
mwingine huduma hiyo hutolewa hadi saa 1:00 usiku kulingana na idadi ya
wateja waliopo katika kituo wakati huo kuanzia Oktoba 18 hadi 24 mwaka
huu.
Zoezi
la kutoa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Surua na Rubella nchini linaongozwa
na kauli mbiu inayosema “Linda, Okoa, Zuia ulemavu- Kamilisha Chanjo”
na kusimamiwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa
ufadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Kusaidia Watoto (unicef), Shirika
la Afya Duniani (WHO), Shirika la Misaada la Marekani (UNSAID) na
Muungano wa watoa chanjo duniani (Gavi).