MY ADVERT EA SHOWBIZ

MY ADVERT EA SHOWBIZ

SIX OFFICE SOLUTION

MOCHRISPO

DARDY FASHION

Oct 22, 2014

MAHAKAMA YA ICC YAIONYA KENYA

Rais wa Kenya, Rais Kenyatta.
Mahakama ya kimataifa ya ICC, imeonya serikali ya Kenya dhidi ya kufichua taarifa kuhusu kesi inayomkabili Rais Uhuru Kenyatta kwa vyombo vya habari nchini humo.
Rais Kenyatta amekuwa Rais wa kwanza aliye mamlakani kufika katika mahakama ya ICC kusikiliza kesi inayomkabili mapema mwezi huu.

Rais wa Kenya, Rais Kenyatta (kulia) akiwa na wakili wake katika Mahakama ya kimataifa ya ICC.
Anakana madai anayokabiliwa nayo ya ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Lakini mahakama inasema kuwa ina wasiwasi kuhusu serikali Kenya kuweza kuficha taarifa kuhusu Kesi ya Kenyatta.
Katika ripoti yake iliyotolewa Jumanne, mahakama hiyo iligusia hatua ya kufichuliwa kwa maelezo au ombi la siri lilitolewa na majaji kwa serikali ya Kenya kuisaidia kupiga tanji mali ya Rais Kenyatta.
Ombi hilo lilitolewa kwa njia ya kisiri hata hivyo maafisa wakuu wa Kenya waliwasilisha stakabadhi hadharani kuhusu ombi hilo lililotolewa mwaka 2013 ingawa mawakili wa Kenyatta waliomba radhi kwa hilo.
Maelezo ya ombi hilo tena yalijitokeza katika vyombo vya habari nchini Kenya kati ya mwezi Aprili na Septemba, mwaka huu katika kile ambacho mahakama imesema ni uvujaji wa taarifa za siri kwa vyombo vya habari hata kabla ya mahakama kujulishwa.
Mahakama hiyo imetoa onyo kwa Kenya kwa kutotii mahakama.
Kenyatta anakabiliwa na makosa 5 kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007 ambapo watu 1,200 waliuawa na wengine laki sita kuachwa bila makao katika ghasia mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Kenya tangu Kenya kujipatia uhuru mwaka 1963.
Tarehe 8 mwezi Oktoba alitakiwa na mahakama kufika ICC kwa kikao maalum.
Lakini wadadisi wanasema kuwa kesi hiyo imegonga mwamba upande wa mashitaka ukituhumu serikali ya Kenya kwa kubana ushahidi unaohitajika na mahakama hiyo huku utetezi ukisema bila ya ushahidi kesi hiyo haipaswi kuendelea.