Mdee na wenzake wanane, waliachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,jijini Dar es Salaam jana baada ya kutimiza masharti ya dhamana katika kesi ya kupinga amri halali ya Jeshi la Polisi na kukusanyika isivyo halali kwa lengo la kwenda Ikulu.
Mbali na Mdee, wengine walioachiwa huru ni Rose Moshi, Renina Leafyagila, Anna Linjewile, Mwanne Kassim, Sophia Fanuel, Edward Julius, Martha Mtiko na Beatus Mmari.
Baada ya kuachiwa kwa dhamana Mdee alisikika akisema ‘people’s na wanachama hao walisikika wakiitikia ‘power’ hali iliyosababisha vurugu kubwa na kuwalazimu askari polisi wenye sare na askari kanzu kuanza kuwatawanya kutoka kwenye viunga vya mahakama.
Hata hivyo, Mdee alisimama ndani ya gari yenye namba za usajili T152 BSR aina ya Toyota V8 ya rangi nyeusi na kuwaambia waandishi wa habari kwamba, alilala mahabusu ya Segerea kimakosa.
“Kama serikali walidhani wamenikomoa kunilaza Segerea ni sawa na bure, kwa sababu nimekula ‘bata’, ambao sijawahi kula huko mahabusu…kama tulikuwa tunachechemea, sasa tunakimbia Chadema,” alisema Mdee nje ya mahakama baada ya kupata dhamana.
Mdee alitoa kauli hiyo huku viunga vya mahakama hiyo vikiwa vimefurika watu wanaodaiwa kuwa wafuasi Chadema, wakati huo huo ulinzi mkali wa askari polisi waliokuwa na silaha za moto, mbwa na gari lenye maji ya kuwasha ukiimarishwa.
Mdee na washtakiwa wenzake walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Janeth Kaluyenda, kwa ajili ya kusikiliza masharti ya dhamana dhidi ya kesi inayowakabili, majira ya saa 6:17 mchana.
Mapema Oktoba 7, mwaka huu, Mdee na washtakiwa wenzake, walishindwa kutimiza masharti ya dhamana, baada ya nyaraka za wadhamini kushindwa kukamilika kufanyiwa uhakiki.
Upande wa Jamhuri jana uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Bernad Kongola, akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Salum Mohamed, na Wakili wa Serikali, Hellen Moshi.
Kongola alidai kuwa Oktoba 4, mwaka huu, katika Mtaa wa Ufipa, uliopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam, isivyo halali, washtakiwa walikiuka amri halali ya Mrakibu wa Polisi (SP), Emmanuel Tillf, iliyowataka kutawanyika.
Ilidaiwa kuwa siku na mahali pa tukio la kwanza, washtakiwa walifanya mkusanyiko isivyo halali kwa lengo la kuandamana kwenda Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Washtakiwa wote walikana mashitaka hayo.
Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuiomba mahakama tarehe ya kusikiliza maelezo ya awali.
Hakimu Kaluyenda alisema washtakiwa watakuwa nje kwa dhamana wakijidhamini kwa kusaini hati ya dhamana ya Sh. milioni moja, kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi katika taasisi zinazotambulika.
Hakimu Kaluyenda alisema kesi hiyo itatajwa Oktoba 21, mwaka huu.
Viunga vya mahakama jana vilifurika na wanaodaiwa kuwa wafuasi Chadema, huku ulinzi mkali wa askari polisi waliokuwa na silaha za moto, mbwa na gari lenye maji ya kuwasha ukiimarishwa.
CHANZO: NIPASHE