Kuna watu ambao wanapata mafanikio makubwa kwa kutumia uchawi. Ila mafanikio yale hayaletwi na uchawi bali imani ya mtu husika.
Tutajadili
kwa nini waganga wanaweza kuwapatia watu wengine dawa au mbinu za kuwa
matajiri wakati wao ni masikini. Na pia tutaangalia jinsi ambavyo
unaweza kutumia mbinu hizi wanazotumia waganga bila ya wewe kuwa mchawi
na ukafikia mafanikio makubwa.
Kila
mmoja wetu anaelewa kwamba kuna watu wanakwenda kwa waganga na
wanasaidiwa kupata utajiri. Japokuwa utajiri huu haudumu, lakini angalau
wanaupata kwa kiwango fulani.
Wakati waganga hawa wanawasaidia watu kuweza kujenga magorofa, wao bado wanakaa kwenye vibanda vya nyasi.
Sasa kwa nini wao wasingetumia uchawi wao na kuwa matajiri zaidi ya hao wateja wao? Ina maana wao hawapendi utajiri huo?
Mbinu za waganga kuwasaidia watu kupata utajiri.
Watu wanaokwenda kwa waganga ili kupata utajiri au mafanikio yoyote hupewa masharti ambayo ni magumu kwa kiasi fulani.
Na
watu hawa huambiwa wakivunja masharti hayo tu utajiri wao unaisha mara
moja. Ni masharti haya ambayo humjengea mtu nidhamu kubwa sana na
kumfanya aweze kufanya kazi kwa juhudi kubwa kuliko wengine ambao
wanafanya anachofanya.
Kwa
mfano mganga anamwambia mtu kila siku aamke asubuhi na mapema sana na
apasue nazi barabarani ndio aende kwenye biashara zake.
Kupasua
nazi hakuna uhusiano wowote na mafanikio yake ila kuamka asubuhi na
mapema kila siku ina msaada mkubwa kwenye mafanikio yake.
Hivyo
mtu huyu atafuata masharti haya kila siku na hata kama kuna siku
hajisikii itambidi afanye tu kwa sababu ameshaaminishwa akiacha
atafilisika.
Sasa
wewe ambaye huna sharti la aina hii siku ukiwa hujisikii vizuri
unalala, siku nyingine unachelewa na hivyo kushindwa kufikia mafanikio
makubwa.
Masharti
mengine kama kutokufanya starehe, kutokunywa pombe, kuvaa nguo moja na
mengine mengi yanapelekea mtu kupunguza matumizi na kupata muda mwingi
wa kufikiria kazi au biashara yake.
Masharti
mengine yanayotolewa na waganga ni kumfanya mtu aweze kuondoka kwenye
woga wake(comfort zone). Kila mmoja wetu kuna vitu fulani anaogopa
kufanya, lakini vitu hivi ndio vinaweza kumletea mafanikio.
Ili kukuondolea woga huu mganga anamfanya mtu afanye jambo kubwa sana ambalo litamuondolea woga kabisa.
Kwa mfano mtu anaambiwa aue, kwa kuona kwamba ameweza kuua mtu, inamfanya mtu asizuiwe na kitu chochote.
Kikubwa
ambacho mganga anamsaidia mtu ni kumjengea utaratibu ambao lazima kila
siku ataufuata na pia kumjengea nidhamu binafsi na hivyo kuweza kufanya
jambo hata kama hajisikii kufanya. Na hili ndio hitaji kubwa la kuweza
kufikia mafanikio.
Kwa nini waganga hawawezi kutumia mbinu hii wenyewe.?
Kwa sababu wanajua inavyofanya kazi na pia hawana mtu wa kuwajengea imani hiyo kubwa kwao wenyewe.
Kwa nini watu baadaye hufilisika?
Wengi
hufilisika baadae kwa sababu wanapopata mafanikio wanasahau kutumia
yale masharti waliyopewa na pia imani yao inakuwa imewekwa kwenye vitu
fulani(mfano hirizi) badala ya kuwa kwao wenyewe.
Ufanyeje ili uweze kutumia mbinu hii kufikia mafanikio.
Cha kwanza kabisa lazima ujijengee nidhamu binafsi. Jiwekee masharti yako ambayo utayafuata kila siku na hakikisha unayafuata.
Kwa mfano weka utaratibu kwamba kila siku utakuwa unaamka saa kumi asubuhi, kuipanga siku yako na kisha kujisomea kidogo.
Baada
ya hapo unawahi kwenye eneo lako la kazi au biashara na kuanza kazi
zako mapema. Pia unaweza kujiwekea utaratibu kwamba kila mteja au mtu
yeyote unayekutana naye kwenye siku husika atajisikia vizuri kukutana na
wewe.
Fuata masharti haya kila siku na utaona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako na shughuli zako.
Kwa hiyo mpaka sasa una mbinu mbili za uhakika za kufikia mafanikio;
1. Una uwezo mkubwa uko ndani yako, ila unatakiwa kuwa na imani kubwa sana kwamba unaweza kupata kile unachotaka.
2.
Lazima uwe na nidhamu binafsi, uwe na masharti(rituals) na uwe na
utaratibu wa kufanya kila siku (routine). Vitu hivi jiwekee mwenyewe na
vifuate kila siku kwenye maisha yako.
Ukiweza kufanya mambo hayo mawili ni lazima utafikia mafanikio makubwa.
Nakutakia
kila la kheri katika kufikia mafanikio. Kumbuka unaweza kufanikiwa kwa
kiwango kikubwa sana bila ya kutumia uchawi au kwenda kwa mganga.Uchawi
kamili upo kwenye kichwa chako. Anza kuutumia sasa.
Makirita Amani-(Amka mtanzania)