Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Rita, Josephat Kimaro, alisema adhabu hiyo imewekwa kwa wale watakaofanya makosa ya kutoa taarifa za uongo ili waweze kupatiwa vyeti vya kuzaliwa au kifo.
Kimaro alisema kwamba adhabu hiyo humpata mkosaji hapo hapo baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa taarifa zake na kulinganisha na zile alizoziwasilisha Rita ili kupatiwa cheti kipya.
"Kifungu namba 28 (3) cha sheria ya kuandikisha vizazi na vifo kimeweka adhabu kwa makosa ya kutoa habari za uongo na adhabu hiyo hutolewa hapo kwa hapo," alisema Kimaro.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo (sura ya 108) toleo la mwaka 2002, ni kosa la jinai kutoa taarifa za uongo kwa Msajili, na pia kosa la jinai kughushi.
Alisema kwa sasa suala la Sitti limepelekwa kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo (Philip Saliboko) na mara baada ya kukamilika taarifa zake zitatolewa hadharani ili jamii ifahamu ukweli.
"Huo mkanganyiko tumeshaupokea na tunaufanyia kazi, tutafanya kazi hii kwa kuzingatia na kufuata sheria na miongozo," Kimaro alisema.
"Rita imebaini kuwapo na udanganyifu wa aina hiyo ambao unafanywa na waombaji kwa kutuma maombi mapya baada ya kutakiwa kupeleka vyeti ili wapate ajira, kujiunga na vyuo au kusafiri nje ya nchi.
~Chanzo: Gazeti la Nipashe