MSANII nyota wa nyimbo za Injili Bongo, Rose Muhando anadaiwa kuingia mitini na shilingi milioni moja alizolipwa kwa ajili ya kutumbuiza kwenye uzinduzi wa albamu ya Injili ya John Lisu iitwayo Uko Hapa, Jumapili iliyopita.
Msanii nyota wa nyimbo za Injili Bongo, Rose Muhando.
Kwa mujibu wa chanzo makini, Rose alimegewa kiasi hicho cha pesa na
Kampuni ya Msama Promotion iliyoandaa uzinduzi huo uliofanyika ndani ya
Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar Jumapili iliyopita.“Rose jamani ana mambo! Mnajua kama amemliza Msama (mkurugenzi wa Msama Promotion) shilingi milioni moja? Alipewa ili atumbuize kwenye uzinduzi wa albamu ya John Lisu lakini akaingia mitini.
“Mbaya zaidi kila alipopigiwa simu kuulizwa kwa nini hajafika Dar ile Jumamosi ili Jumapili awepo ukumbini akawa hapokei simu.
Kikaendeela: “Rose ananishangaza sana, sikuwahi kufikiria kama anaweza kufanya hivyo, kikubwa kinachowaumiza wengi ni kutopokea simu na ingekuwa vizuri kama angetoa taarifa mapema kwa kutohudhuria kwake na sisi tungejua cha kufanya mapema,” kilisema chanzo hicho ambacho kipo ndani ya waandaaji hao.
Chanzo hicho hakikuishia hapo, kiliendelea kuanika kuwa shutuma za aina hiyo zimekuwa zikimuandama sana mwanamuziki huyo kiasi cha kushindwa kuaminika na kudai kuwa hana njaa ya kutokomea na pesa hiyo kwani ni kiasi kidogo sana kwake.
Msanii nyota wa nyimbo za Injili Bongo, Rose Muhando akizungumza jambo.
Risasi Mchanganyiko lilimsaka bosi wa Msama Promotion, Alex Msama
ambaye alikiri Rose kutotokea kwenye uzinduzi huo licha ya kulipwa kiasi
hicho cha pesa na kilichomuumiza zaidi ni kutopokea simu za wasaidizi
wake waliotaka kujua nini kilimpata.“Aliniangusha sana maana hata yeye nilimtangaza sana kwenye vyombo vya habari kwamba atakuwepo, lakini matokeo yake ikawa kimya, sijui nini kimempata lakini nitatoa tamko siku mbili hizi,” alisema Msama kwa masikitiko makubwa.
Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Rose Muhando kupitia simu yake ya kiganjani, alipokea na mambo yalikuwa hivi.
Mwandishi: Habari yako dada Rose?
Rose: Nzuri tu habari yako wewe
Mwandishi: Nzuri, mimi ni (akataja jina lake)
Rose: Hilo jina siyo geni kwangu.
Mwandishi: Mimi ni mwandishi wa Global.
Rose: Ahaaa, subiri kidogo nitoke nje niko benki nitakupigia.
Baada ya kukata simu, Rose alikaa kimya kwa zaidi ya dakika tano. Mwandishi wetu alipopiga tena mara kadhaa simu yake haikupokelewa
CHANZO GLOBAL PUBLISHER