Mkurugenzi
Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi
na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues aliposimama kwenye
Kijiji cha Ngeresero kwa ajili ya kuwaungisha wanawake wa kimasai
wanaofanya biashara ya kuuza bidhaa mbalimbali za shanga kwa watalii
wanaosimama kwenye kijiji hicho kwa ajili ya kupata mahitaji mbalimbali,
wakati akielekea kijiji cha Ololosokwan kilichopo wilayani Ngorongoro
mkoani Arusha kukagua miradi mbalimbali inayofadhiliwa na shirika lake
la UNESCO.
NDOTO
ya kuwa na kijiji cha dijitali nchini Tanzania itaanza kutimia Januari
mwakani wakati vifaa vinavyotakiwa kukamilisha mradi huo vitakapowasili
kutoka kampuni ya Samsung Electronics.
Kwa
mujibu wa watekelezaji wa mradi huo mkubwa unaotarajiwa kutumia dola za
Marekani milioni 1, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na
Utamaduni (UNESCO) vifaa hivyo vinatarajiwa kuingia Bandari ya Dar es
Salaam Januari tano mwakani.
Mkataba
wa kuanzishwa kwa kijiji cha dijitali eneo la Ololosokwan tarafa ya
Loliondo wilayani Ngorongoro ulitiwa saini kati ya Unesco na Samsung
electronics Novemba 6 mwaka huu.
Akizungumza
na halmashauri ya kijiji cha Ololosokwan , Mkurugenzi Mkazi wa Shirika
la UNESCO Tanzania, Zulmira Rodrigues amewataka wanakijiji kujiandaa
kwa mabadiliko makubwa ya kijiji chao kinapoingia katika dunia ya
dijitali.
Alisema
mambo ambayo wanastahili kuyaweka sawa ili kufanikisha ndoto zao
kuhakikisha eneo ambalo mitambo na miundombinu ya mradi ipo ni lazima
lisajiliwe kisheria ili kusiwepo na tatizo katika siku za usoni.
Aidha
kutokana na ukubwa wa mashine zinazohusika, hasa makontena ni vyema
wanakijiji wakaangalia maeneo korofi katika barabara za kuelekea huko na
kuzirekebisha, ili magari hayo makubwa yenye vifaa yapite kwa usalama.
Alisema mradi huo wa miaka mitatu unatarajia kuwawezesha wananchi wa
eneo hilo kuwa na ujasirimali, matumizi ya teknolojia ya kisasa katika
mawasiliano na utafutaji wa masoko, elimu na afya.Kwa mujibu wa Bi.
Rodrigues kijiji hicho pia kitakuwa na shule iliyoungwa na mtandao wa
kompyuta duniani (intaneti), kliniki ya kisasa, tiba kwa kutumia
teknolojia ya kompyuta na jenereta kubwa linalotumia nishati ya jua.
Bw. Abdulaziz Ali wa kitengo cha Transportation and Logistic kutoka
UNESCO akitafsiri bei za bidhaa hizo za kimasai kwa wakimama hao
wanaofanya biashara za urembo wa shanga kwa watalii na wazawa wanaopita
katika kituo kijiji hicho ambapo wengine wao husimama kupata huduma ya
chakula na vinywaji.
Aidha
kuwapo na mtandao wa kompyuta kutawezesha UNESCO kwa kushirikiana na
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuanzisha mtaala utakaowawezesha
vijana wa kimasai ambao ni wafugaji kupata elimu wanayoihitaji.
Mwakilishi huyo wa UNESCO amesema kwamba amefurahishwa na namna watu
walivyoitikia mradi huo ambao umelenga kubadili maisha ya wafugaji hao
kwa kuwawezesha pia kuitumia vilivyo sekta ya utalii. “Kupitia mradi huu
wananchi wanaweza kujifunza kusoma, kupata maarifa na katika harakati
hizo kujua lugha ya kiingereza ili kuwasaidia kuwa na mawasiliano na
watalii na watu wengine”, alisema Rodrigues.