Bingwa wa zamani wa michuano ya gofu
ya wazi ya Uganda, Mtanzania Angel Eaton amesema yuko tayari kwa ajili
ya kushiriki Olimpiki ya mwakani lakini angependa kupumzika kidogo.
“Mwaka jana nimecheza michuano mengi, na mwaka ndio kwanza umeanza ila ningependa nipumzike kidogo”.“Najua mwakani kuna michuano ya Olimpiki huko Brazil, nitakuwa tayari kushiriki katika timu endapo nitachaguliwa”, alisema Eaton.
Eaton ni mmoja wa wachezaji mahiri nchini Tanzania na mwaka jana alipoteza taji la wazi la Uganda kwa mpinzani wake Flaviana Namakula wa Uganda.
Endapo Eaton angeshinda, basi hiyo ingekuwa ni mara yake ya tatu (hat-trick) kushinda michuano hiyo kwa mfululizo.
Golf inategemewa kuwa ni sehemu ya michuano ya Olimpiki baada ya kuwa nje kwa karne nyingi, ikiungana na mchezo wa raga.
Kwa mujibu wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), michuano ya kufuzu kucheza Olimpiki kwa nchi za Afrika ya Mashariki (Kanda ya 5) itafanyika Kigali, Rwanda mwezi wa kumi mwaka huu.