MY ADVERT EA SHOWBIZ

MY ADVERT EA SHOWBIZ

SIX OFFICE SOLUTION

MOCHRISPO

DARDY FASHION

Mar 12, 2015

VIJIJI 10 VYANUFAIKA NA UMEME JUA KUTOKA WIZARA YA NISHATI NA MADINI

Baadhi ya watalaam kutoka Kampuni ya Elektro Merl ya nchini Austria ambao walileta na kufunga makontena ya umeme wa jua pamoja na mfumo wa usambazaji umeme kwa vijiji 10 vilivyo mbali na gridi ya taifa, pamoja na baadhi ya wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini, wakikagua moja ya makontena ya umeme wa jua katika Kijiji cha Lobilo, wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma hivi karibuni.
Baadhi ya nyumba za wananchi katika Vijiji vya Lobilo na Silale, wilayani Kongwa, mkoa wa Dodoma, zilizounganishiwa huduma ya umeme wa jua kupitia makontena maalum.
Taa zilizofungwa mtaani/barabarani katika Vijiji vya Lobilo la Silale, wilayani Kongwa, mkoa wa Dodoma. Taa hizi zinazotumia umeme wa jua na ni sehemu ya mradi wa makontena ya umeme wa jua.
Jengo lenye vyumba vya biashara mbalimbali ikiwemo saluni ya kukata nywele lililo katika Kijiji cha Lobilo, wilayani Kongwa mkoa wa Dodoma. Biashara hizi zinazotegemea umeme, zimewasaidia wananchi mbalimbali kuinua kipato na kuboresha maisha yao. Wananchi wa kijiji hiki wamenufaika na huduma ya umeme kutokana na makontena ya umeme wa jua.
Kutoka Kushoto ni Mhandisi Stephan Kashushura (Wizara ya Nishati na Madini), Mhandisi Hannes Merl (Kampuni ya Elektro Merl), Mhandisi Styden Rwebangira (Wizara ya Nishati na Madini), na Paul Kiwele (Wizara ya Nishati na Madini), wakijadiliana namna ya kuboresha mradi wa makontena ya umeme wa jua, awamu ya pili, baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza. Hapa ni katika Kijiji cha Lobelo kilichoko wilayani Kongwa, mkoa wa Dodoma.

Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Kampuni ya Elektro Merl, wakijadiliana namna ya kuboresha mradi wa makontena ya umeme wa jua - awamu ya pili, baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza. Mradi huo unalenga kuwapatia umeme wananchi wa vijiji vilivyo mbali na gridi ya taifa na tayari, vijiji 10 vimenufaika kupitia mradi huo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Lobelo kilichoko Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, Alex Ngulele (mwenye kofia), akitoa shukrani kwa Maofisa wa Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Wataalam kutoka Kampuni ya Elektro Merl kwa kufungiwa umeme katika Kijiji chake.
Makontena ya umeme wa jua yaliyopo katika Vijiji vya Lobilo na Silale, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Makontena haya ni sehemu ya Mradi unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, ambapo upo katika hatua ya majaribio na unalenga kuvipatia umeme vijiji vilivyo mbali na mfumo wa gridi ya Taifa.
Taa ikiwaka ndani ya nyumba ya Stephano Manzo, mkazi wa Kijiji cha Silale, wilayani Kongwa, mkoa wa Dodoma. Nyumba hii ni miongoni mwa kaya zilizounganishiwa huduma ya umeme kupitia mradi wa makontena ya umeme wa jua.
Na Veronica Simba – Dodoma
Jumla ya Vijiji 10 katika Wilaya za Kongwa, Mlele na Uyui vimeunganishiwa umeme kupitia Mradi wa makontena ya kuzalisha umeme kutokana na jua.
Mradi huo unatekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, ambapo upo katika hatua ya majaribio na unalenga kuvipatia umeme vijiji vilivyo mbali na mfumo wa gridi ya Taifa.
Wizara ya Nishati na Madini wiki hii, ilisaini makubaliano ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya Mradi na Kampuni ya Elektro-Merl ya nchini Austria ambayo ndiyo ilileta na kufunga makontena 14 ya umeme wa jua pamoja na mfumo wa usambazaji umeme kwa nyumba zilizoko katika vijiji husika.
Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo, Mwakilishi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Styden Rwebangira alisema wananchi waliounganishiwa umeme huo wa jua, watapata huduma hiyo bure kwa kipindi cha miaka miwili ya mwanzo ambayo ni ya matazamio.
Alisema kuwa, baada ya miaka miwili, kuanzia tarehe waliyosaini makubaliano, wananchi wa vijiji husika wataanza kuchangia fedha kidogo kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali kama betri na paneli vinavyotumika katika mradi huo, ambavyo vina ukomo wa kutumika.
“Vifaa hivi vina gharama kubwa sana, hivyo inabidi kuwa na utaratibu wa kukusanya fedha za kutosha ili kuweza kununua vifaa vingine pindi vilivyopo vinapofikia ukomo wake wa kutumika. Hivyo kila mwananchi anayetumia huduma hii inabidi achangie gharama,” alisema Mhandisi Rwebangira.
Aidha, aliongeza kuwa, ili kuhakikisha mradi unatoa matokeo yaliyotarajiwa, inabidi uendeshwe na mtu au kampuni yenye utaalamu wa masuala ya umeme, mitambo ya umeme jua pamoja na uzoefu na ufahamu wa kutosha kuhusu mitambo ya aina hiyo.
“Hivyo, kila baada ya miaka miwili, ukiacha kipindi cha majaribio ambapo mradi utakuwa chini ya Wizara, atachaguliwa mtaalamu au kampuni kupitia njia ya ushindani ambaye atalipwa kwa utaratibu utakaokubaliwa katika mkataba,” alisema Rwebangira.
Kwa upande wake, Ofisa wa Wizara aliyefika kushuhudia utiaji saini makubaliano ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi, Paul Kiwele alisema Wizara ilifanya tathmini ya kuchagua vijiji kwa ajili ya majaribio ya mradi huo ambapo vigezo mbalimbali vilitumika.
Kiwele alivitaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na Kijiji husika kuwa mbali na gridi ya Taifa, kutokuwa katika mpango wa kufikiwa na miradi ya umeme ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) hivi karibuni.
Alitaja vigezo vingine kuwa ni nyumba za Kijiji husika kuwa karibu pamoja na uwepo wa matumizi ya kiwango cha umeme utakaozalishwa.
“Aidha, kwa kuwa mradi huu ni wa majaribio, ililengwa kupata mikoa mitatu tofauti ili uzoefu utakaopatikana utumike katika uendelezaji teknolojia hii katika maeneo mengine ya nchi,” alisema.
Naye, Mtaalam kutoka Kampuni ya Elektro Merl, Mhandisi Hannes Merl akizungumzia mkataba uliosainiwa na Wizara pamoja na Kampuni yake, Januari mwaka jana kuhusu utekelezaji wa mradi husika, alisema mbali na kufunga makontena 14 ya umeme wa jua pamoja na mfumo wa usambazaji umeme, mkataba pia ulihusisha ufungaji wa waya, taa, swichi na soketi moja kwa kila nyumba iliyofikiwa.
Mhandisi Merl alisema kila kontena lina uwezo wa kuzalisha kWp 13.75 ambapo kila nyumba ya makazi na huduma za biashara zimetengewa W 250 na taasisi za kijamii zimetengewa W 500.
Aliongeza kuwa, wananchi wanaweza kuunganisha mashine ndogo ndogo za kusaga, kuchomelea, kuranda na kuchana mbao pamoja na nyinginezo kutoka katika makontena hayo hivyo kunufaika na shughuli za kiuchumi.
Pia, Mhandisi Merl alisema mradi umetoa jokofu kwa kila zahanati na vituo vya afya vilivyopo katika vijiji vinavyonufaika na mradi huu. Aidha, alisema kuwa mradi umefunga taa za mitaani kwa kila kijiji kitakachonufaika na mradi husika.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi katika vijiji vilivyonufaika na mradi huo wa makontena ya umeme wa jua, waliishukuru na kuipongeza Serikali kwa wazo zuri la kuwapelekea wananchi hao umeme wa jua ili nao waweze kunufaika kwa namna mbalimbali kutokana na uwepo wa nishati hiyo muhimu.
“Ninaishukuru sana Wizara ya Nishati na Madini kuona matatizo yetu na kusikia kilio chetu. Imekuwa kama ndoto. Umeme huu umeniwezesha kuendesha biashara ya saluni kwa njia ya kisasa kabisa. Situmii tena Mkasi kunyoa wateja wangu kama hapo awali. Sasa ninatumia mashine za kunyolea na ninapata wateja wengi, hivyo kuboresha kipato changu na maisha yangu kwa ujumla,” alisema Lazaro Kutamika, mkazi wa Kijiji cha Lobilo, Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma.
Wizara ya Nishati na Madini imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali katika jitihada za kuwafikishia wananchi huduma ya umeme. Kwa kupitia mradi huo wa makontena ya kuzalisha umeme kutokana na jua, Serikali inafanya majaribio ya kuvipatia umeme vijiji vilivyo mbali na mfumo wa gridi ya Taifa kwa kutumia teknolojia husika.
Vijiji vilivyonufaika na mradi huo kwa awamu ya kwanza ni pamoja na Lobilo, Leganga, Ngutoto na Silale vya mkoa wa Dodoma. Vingine ni Tura, Loya na Lutende vilivyoko mkoa wa Tabora. Aidha, kwa mkoa wa Katavi, vijiji vilivyonufaika ni Nsenkwa, Mapili na Ilunde. 

HABARI KWA HISANI YA MICHUZI BLOG