Mshambuliaji
wa timu ya wasichana wa Temeke Christina Daudi (kushoto) akimtoka beki
wa Arusha Vailet Valerian wakati timu hizo zilipokutana katika ufunguzi
wa michuano ya Airtel Rising Stars kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume
jijini Dar es Salaam Temeke walishinda magoli 8-0.
Mchezaji
wa timu ya wasichana wa Temeke Madelin Enock (kushoto) akiwania mpira
na mchezaji wa Arusha Mariam Rashid wakati timu hizo zilipokutana katika
ufunguzi wa michuano ya Airtel Rising Stars kwenye uwanja wa Kumbukumbu
ya Karume jijini Dar es Salaa jana. Temeke walishinda magoli 8-0.
Beki wa timu ya wasichana wa
Temeke Eva Wailes, akiwatoka wachezaji wa Arusha wakati timu hizo
zilipokutana katika ufunguzi wa michuano ya Airtel Rising Stars kwenye
uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam jana. Temeke
walishinda magoli 8-0.
Pazia la michuano Taifa ya soka ya
vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars jana
lilifunguliwa katika uwanja wa Kukumbukumbu ya Karume jijini Dar es
Salaam ambapo timu ya wasichana ya Temeke ilitoa onyo kali kwa timu
shiriki kwa kuifunga Arusha 8-0.
Mchezo huo ulifuatiwa na mechi ya
wavulana kati ya Mwanza na Kinondoni na Mwanza kuibuka na ushindi wa
goli 1-0. Goli la Mwanza lilifungwa na Lazaro Richard katika dakika ya
42 kufuatia krosi iliyopigwa kutoka upande wa kushoto.
Katika mchezo wa kwanza, Temeke walianza
kwa kasi ya aina yake na kupeleka mashambuliazi ya mara kwa mara
langoni mwa Arusha huku Arusha wakionekana kuzidiwa katika kila idara.
Temeke waliandika bao la kwanza kupitia
kwa Oppah Clement kaika dakika ya 24, baada ya kuwahadaa mabeki wa
Arusha na kuachia shuti kali ambalo lilimshinda kipa wa Arusha.
Temeke awalipata bao lao la pili kupitia
kwa Rose Mpoma mnamo dakika ya 27 ambaye aligongeana mpira kwa uzuri na
Oppah Clement na kisha kumchambua kipa wa Arusha kwa umaridadi wa hali
ya juu na kuukwamisha mpira huo kimiani.
Alikuwa ni Oppah Clement tena, ambaye
aliiandikia Temeka bao la tatu mnamo dakika ya 28 baada ya kuunganisha
krosi iliyochongwa na Shamimu Hamisi kutoka upande wa kushoto mwa uwanja
na kuendeleza karamu ya magoli kwa Temeke.
Shamimu Hamisi aliifungia Temeke bao la
nne katika dakika ya 51 na kuzidi kuzamisha jahazi la Arusha ambao
walinekana kama vile wamesimama wakati mchezo ukiendelea.
Rosea Mpoma aliwaliza kwa mara nyingine
tena Arusha baada ya kuifungia Temeke bao la tano katika dakika ya 53
baada ya kuachia shuti kali na kuzama moja kwa moja wavuni.
Temeke waliendeleza kupeleka kilio kwa
Arusha baada ya Asia Juma kufunga goli la sita na la saba baada ya
kuwatoka mabeki wa Arusha kwa nyakati tofauti na kuwapa raha mshabiki
wao.
Shamimu Hamisi alihitimisha karamu ya
magoli kwa Temeke baada ya kufunga bao la nane na kuamsha nderemo na
vifijo kwa maelfu ya mashabiki wao waliohudhura uwanjani hapa.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Temeke
Daudi Siang’a alisema kuwa walistahili kushinda kutokana na kuwaandaa
vijana wake kikamilifu kwa ajili ya mashindano haya, hivyo haoni kama
kuna timu ya kuwazuia msimu huu.
“Timu yangu ilicheza vizuri na
ilistahili ushindi kwa sababu kisaikolojia wachezajji wangu wako vizuri,
lakini vile vile niliwapa muda mrefu wa maandalizi yenye mbinu
madhubuti, kwa ushindi wa leo kwetu si wa kubahatisha”, alisema Siang’a.
Kwa upande wake, kocha wa Arusha Gefrey
Mrope alisema kuwa, hofu ya mashindano juu ya vijana wake ndio sababu
kubwa ya kupoteza mchezo wa leo kwa kuungwa idadi kubwa ya mabao lakini
aliaahidi kufanya marekebishao katika hilo.
“Kisaikolojia wachezaji wangu wengi ni
wapya hivyo hawana uzoefu wa kucheza katika kadamnasi kubwa ya watu kama
hii, lakini naahidi kulifanyia kazi jambo hilo ili katika mchezo ujao,
tuweze kupata ushindi”, alisema Mrope
habari na GPL