Moja kati ya machimbo ya dhahabu mkoni Geita
Watu wanne wamepoteza maisha
na wengine watatu kujeruhiwa baada ya kufukiwa na kifusi katika machbo
ya Nyamalinde kijiji cha Sobola nje kidogo ya wilaya ya Geita, mkoani
Geita. Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo amesema tukio hilo
limetokea leo majira ya saa mbili asubuhi katika machimbo hayo
yanayomilikiwa na wananchi licha ya kuwa tayari yalishapigwa marufuku
kuendelea kwa kazi hiyo.
Mponjoli amesema tukio hilo limetokea
baada ya watu 7 kuingia ndani ya mgodi huo, lakini muda mfupi baadaye
kifusi kikawaangukia na kusababisha vifo vya watu wanne kati yao huku
watatu wakitoka salama licha ya kuwa na majeraha.
Amewataja watu waliopoteza maisha kuwa ni pamoja na Robert Kazegemwa, Jeremia Emmanuel, Makenya Mwita na Julius Timotheo.
Waliojeruhiwa ni pamoja na Mashaka Samuel, Justine Safari na Maneno Lusika ambao wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Katoro.
Katika tukio lingine, leo majira ya saa
7 mchana tetemeko dogo la ardhi limetikisa katika mkoa wa Geita ambapo
licha ya kutokuwa na madhara yoyote, limezua taharuki katika maeneo
mbalimbali ikiwemo katika shule ya sekondari Nyang'wale.
Kamanda Mponjoli amesema katika shule
hiyo, wanafunzi walikuwa katika mitihani na ndipo walipokimbia kutoka
darasani ili kujiokoa ambapo kutokana na msukumano, mwanafunzi mmoja
alijeruhiwa lakini tayari amekwishapatiwa matibabu na yuko salama